Afrika Kusini yalaani mashambulizi ya kigaidi nchini Syria
Serikali ya Afrika Kusini imelaani vikali mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea hivi karibuni nchini Syria.
Shirika la habari la Xihnua limemnukuu Clayson Monyela, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini akisema katika taarifa ya leo Jumatano kwamba nchi yake inalaani vikali mashambulizi hayo ya kigaidi huko Syria na inawataka watu wote wanaopenda amani duniani, wasimame imara kukabiliana na ugaidi na misimamo mikali.
Monyela aidha amezitaka pande zinazoshiriki katika mazungumzo ya Geneva, Uswisi kuhusiana na Syria wafanye juhudi zao zote kuhakikisha utulivu unarejea nchini humo.
Ikumbukwe kuwa Jumatatu wiki hii, genge la kigaidi la Daesh (ISIS) lilifanya mashambulizi ya miripuko mikubwa katika miji ya bandari ya Jableh na Tartus katika viunga vya Latakia, magharibi mwa Syria na kuua raia zaidi ya 100 wa kawaida na kujeruhi wengine zaidi ya 120.
Mgogoro wa Syria ulinza mwaka 2011 baada ya magenge ya kitakfiri yanayoungwa mkono na madola ya kigeni kuivamia nchi hiyo kwa uungaji mkono wa Marekani na waitifaki wake kwa nia ya kuipundua serikali Rais Bashar al Assad iliyoko madarakani kwa ridhaa ya wananchi.
Magenge hayo yameshafanya jinai kubwa sana dhidi ya raia na maafisa wa serikali pamoja na miundombinu ya Syria.