Syria yaipongeza AU kwa kusimamisha uanachama wa Israel katika jumuiya hiyo
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Syria imekaribisha uamuzi wa Umoja wa Afrika wa kusimamisha hadhi ya uanachama mwangalizi ya utawala wa Kizayuni Israel katika jumuiya hiyo.
Duru rasmi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesema kuwa, uamuzi wa Umoja wa Afrika wa kuusimamisha utawala wa Kizayuni kuwa mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika unadhihirisha msimamo imara wa umoja huo katika kutetea kadhia ya haki ya Palestina.
Chanzo cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria kimeeleza kuwa, hatua hiyo ya Umoja wa Afrika pia imedhihirisha jinsi utawala ghasibu wa Israel unavyozidi kutengwa na imepinga siasa za kichokozi na za kibaguzi za utawala huo, ambazo zinakiuka waziwazi sheria za kimataifa.
Katika kikao chao cha juzi Jumapili huko Addis Ababa, Ethiopia, viongozi wa nchi za Afrika walisimamisha hadhi ya mwanachama mwangalizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika umoja huo na kuunda kamati inayojumuisha wakuu wa nchi saba za Afrika, ikiwemo Algeria, kushughulikia suala hilo.
Harakati za mapambano ya ukombozi za Palestina za Hamas na Jihad Islami zimeushukuru Umoja wa Afrika (AU) kwa kuutimua utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye umoja huo na kusema kuwa, hatua hiyo ni pigo kwa zile nchi zinazotangaza uhusiano wa kawaida na utawala huo katili.
Vilevile Bunge la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imepongeza msimamo wa kihistoria wa Umoja wa Afrika wa kuunga mkono malengo matukufu ya Palestina na kueleza kwamba, uamuzi wa kukataa Israel kupatiwa hadhi ya mwanachama mwangalizi katika umoja huo ni ushahidi tosha wa kuunga mkono haki ya taifa la Palestina.