Chama cha Fat'h: Marekani inashirikiana na Israel kuwakandamiza Wapalestina
Katibu wa Kamati Kuu ya chama cha Fat'h cha Palestina amesema kuwa, eneo la Sheikh Jarrah na maeneo mengine ya Quds yanayokaliwa kwa mabavu, yanaendelea kushuhudia vitendo vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni wa Israel na kwamba jinai hizo zinafanyika kwa uungaji mkono kamili wa Marekani.
Jibril Rajoub amenukuliwa na televisheni ya "al Ikhbaria" ya Syria akisema hayo na kusisitiza kuwa, anawashukuru sana wananchi wa Syria kwa kuwapa hifadhi wakimbizi wa Palestina, kuwapa utambulisho na kuwafungulia njia za kufanya harakati zao kwa uhuru kamili.
Amma kuhusu hali mbaya ya eneo la Sheikh Jarrah na maeneo mengine ya mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, Katibu wa Kamati Kuu ya Chama cha Fat'h cha Palestina amesema, utawala wa Kizayuni unafanya njama za kuteka kila shibri ya ardhi ya Palestina kupitia kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kubadilisha kabisa muundo wa kijiografia na kijamii wa Palestina.
Amesema, kila shibri ya ardhi ya Palestina, Quds na Wapalestina wote ni shabaha ya ukandamizaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel hata kama kwa hivi sasa eneo la Sheikh Jarrah na maeneo mengine ya Wapalestina huko Quds ndiyo yaliyoelemewa zaidi na vitendo vya kigaidi vya Israel huku jamii ya kimataifa ikiendelea kunyamazia kimya jinai hizo.
Jibril Rajoub amewataka wananchi wa Palestina waendeleze muqawama na kusimama kidete akisisitiza kuwa, juhudi zao zote ni kuhakikisha wanakabiliana na Wazayuni kwa kutumia mbinu zote za muqawama na kusimama imara Wapalestina popote walipo, iwe ni Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan au Ukanda wa Ghaza au katika mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.