HAMAS: Israel inacheza na moto kwa kuwakandamiza mateka Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i80994-hamas_israel_inacheza_na_moto_kwa_kuwakandamiza_mateka_wapalestina
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetahadharisha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unacheza na moto kwa kuzidisha mbinyo na ukandamizaji dhidi ya mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela na magereza ya utawala huo pandikizi. 
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 03, 2022 23:12 UTC
  • HAMAS: Israel inacheza na moto kwa kuwakandamiza mateka Wapalestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetahadharisha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unacheza na moto kwa kuzidisha mbinyo na ukandamizaji dhidi ya mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela na magereza ya utawala huo pandikizi. 

Hussein Abu Kwik, kiongozi wa ngazi ya juu wa HAMAS alisema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, "tunafuatilia kwa karibu hali ya wafungwa wa Kipalestina. Katu hatutawaacha peke yao."

Amebainisha kuwa, harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu haitanyamazia kimya jinai na dhulma hizo za Wazayuni dhidi ya mateka wa Kipalestina wanaozuiliwa katika mazingira ya kuogofya.

Ukandamizaji huo wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya mateka Wapalestina umepelekea wananchi wa Palestina wafanye maandamano mara kadhaa ya kutangaza uungaji mkono wao kwa wafungwa hao, huku baadhi ya wafungwa wenyewe wakifanya mgomo wa kula kulaani mbinyo dhidi yao.

 

Wapalestina wanavyofanyiwa unyama na wanajeshi wa Kizayuni

Takwimu zinaonyesha kuwa, kamatakamata hiyo na kuwaweka kizuizini Wapalestina, si tu haijaweza kupunguza nguvu ya operesheni za muqawama, lakini katika mwaka uliopita, opereseni hizo dhidi ya uzayuni zimeongezeka kwa kiwango kikubwa.

Wapalestina zaidi ya 4500 wanashikilia na kuzuiliwa katika jela na magereza mbalimbali ya utawala pandikizi wa Israel unaokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa.