Wabahrain waandamana kulaani safari ya mkuu wa majeshi ya Israel
Wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano ya kulaani safari ya Luteni Jenerali Aviv Kochavi, Mkuu wa Majeshi ya Israel nchini humo, sanjari na kulaani hatua ya utawala wa Aal-Khalifa wa nchi hiyo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
Waandamanaji hao wamesema safari ya mkuu huyo wa majeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel huko Manama mji mkuu wa Bahrain ni usaliti wa utawala wa Aal Khalifa kwa watu wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, safari hiyo inakiuka maadili na ni kitendo chenye lengo la kuyachochea mataifa ya Kiarabu na Kiislamu.
Katika safari hiyo, mkuu huyo wa majeshi ya Israel alikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Ulinzi la Bahrain, Sheikh Nasser bin Hamad Aal Khalifah, na maafiasa wengine wa ngazi za juu wa jeshi la nchi hiyo ya Kiarabu.
Maandamano hayo yamejiri licha ya ukandamizaji wa maafisa usalama na sheria kali ambazo zimewekwa na vyombo vya usalama nchini humo dhidi ya wapinzani wa utawala wa kiukoo wa Aal Khalifa.
Wananchi wa Bahrain wameapa kuendelea kutetea na kuunga mkono malengo ya Palestina, wakisisitiza kwamba hawaafiki hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel.
Mwezi uliopita pia, waandamanaji wenye hasira nchini Bahrain waliteketeza kwa moto bendera za utawala wa Kizayuni wa Israel wakilaani safari ya siku mbili ya Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Naftali Bennet katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.