Hizbullah: Marekani, mchochezi wa migogoro Asia Magharibi na kote duniani
Ofisa mwandamizi wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema Marekani inabeba dhima ya kuanzisha na kuchochea migogoro yote inayoshuhudiwa hivi sasa katika eneo la Asia Magharibi na maeneo mengine duniani.
Sheikh Ali Damoush, Makamu wa Rais wa Baraza Kuu la Hizbullah alisema hayo katika hafla moja iliyofanyika jana usiku mjini Beirut na kuongeza kuwa: Marekani imehusika na misukosuko na ukosefu wa uthabiti katika eneo. Ndani ya miaka 8 iliyopita, Washington imekuwa ikiibua migogoro, kuchochea vita na kuunga mkono ugaidi kote duniani.
Sheikh Damoush ameeleza kuwa, Marekani inabeba dhima pia ya mgogoro wa Ukraine, na matokeo yote hasi kwa dunia yanayotokana na mgogoro huo.
Makamu wa Rais wa Baraza Kuu la Hizbullah ameashiria mgogoro wa kiuchumi wa Lebanon na kueleza kuwa, vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi ya Marekani dhidi ya Beirut ni kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amesema, "Marekani na waitifaki wake kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakiingilia masuala ya ndani ya Lebanon. Washington itashadidisha mashinikizo yake dhidi ya Beirut katika wiki chache zijazo, kwa shabaha ya kuwaunga mkono vibaraka wao katika uchaguzi ujao wa Bunge."
Ofisa huyo mwandamizi wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, uchaguzi huo wa Bunge bila shaka utaihami kambi ya muqawama na utahudumia maslahi ya taifa la Lebanon.