UN yapasisha azimio kulaani jinai za Israel eneo la Golan
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio lililoukosoa vikali utawala wa Kizayuni wa Israel kwa jinai ulizozifanya katika Miinuko ya Golan ya Syria.
Baraza hilo la UN lenye makao yake mjini Geneva lilipasisha azimio hilo katika kikao chake cha kawaida cha 49 Ijumaa, ambapo pia limeitaka Tel Aviv ifungamane na maazimio ya umoja huo.
Aidha baraza hilo kupitia azimio tofauti, kwa mara nyingine tena limelaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel, hususan Quds Mashariki.
Maazimio hayo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yameitaka Israel ikomeshe ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi, sanjari na kuacha kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na Miinuko ya Golan ya Syria.
Baraza hilo la UN limesema wananchi wa Palestina wana haki ya kuishi kwa uhuru ndani ya ardhi yao, kufanyiwa uadilifu, na kuheshimiwa haki ya taifa lao huru la Palestina.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwakilishi wa Kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa, Hussam Eddin Ala amesema utawala wa Kizayuni wa Israel unakiuka sheria za kimataifa na haki za binadamu kwa uungaji mkono kamili wa Marekani.
Amesema Israel inapaswa kuadhibiwa kwa jinai zake za kimfumo, kama kupora ardhi na rasilimali za Wasyria katika eneo la Golan, ambayo ni milki ya Syria kwa mujibu wa maazimio na sheria za kimataifa, na kuongeza kuwa lazima eneo hilo lirejee chini ya mamlaka ya Syria, katika mpaka wa tarehe 4 Juni mwaka 1967.