"Mapambano ya Wapalestina yameingia katika marhala mpya"
Mkuu wa Kituo cha Intifadha ya Palestina na Quds katika Baraza la Kuratibu Tablighi ya Kiislamu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Mapambano ya Wapalestina dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yameingia katika marhala mpya.
Ramadhan Sharif alisema hayo jana Jumapili katika mkutano uliofanyika hapa Tehran na kueleza kuwa, mchakato wa kufanya mazungumzo na kujaribu kufikia mwafaka na utawala haramu wa Israel umeshindwa kuzaa matunda, jambo ambalo limewasukuma Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wajiunge na wenzao wa Gaza kuendelesha mapambano dhidi ya Tel Aviv.
Jenerali Ramadhan Sharif amesema taifa la Palestina limechoshwa na kutamaushwa na mazungumzo marefu ya kujaribu kupatanishwa na Israel, na hivi sasa limeamua kufungua ukurasa mpya wa mapambano yake.
Mkuu wa Kituo cha Intifadha ya Palestina na Quds katika Baraza la Kuratibu Tablighi ya Kiislamu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, operesheni za makundi ya muqawama huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu zimeyumbisha na kudhoofisha usalama wa Israel, mbali na kuutia kiwewe utawala huo wa Kizayuni.
Amesema operesheni za wanajihadi na wanamuqawama wa Palestina hitimaye zitaufanya utawala ghasibu wa Israel upoteze utambilisho wake, na kuwa chachu ya kuharakisha mchakato wa kuporomoka utawala huo pandikizi.
Katika siku za hivi karibuni, vijana wa Kipalestina wameshadidisha operesheni za kujitolea kufa shahidi katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni, ambapo Wazayuni kadhaa wameangamizwa.