Kuendelea hatua za Imarati dhidi ya taifa la Palestina
Ikiwa ni katika kuendeleza hatua zake dhidi ya taifa la Palestina na katika kivuli cha kudumushwa vitendo vya mabavu vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina, serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati, imechukua hatua nyingine mbili katika kuimarisha uhusiano wake na utawala huo wa kibaguzi.
Katika miaka miwili iliyopita, Imarati imekuwa mstari wa mbele kati ya nchi za Kiarabu katika kuimarisha uhusiano wake na utawala haramu wa Israel. Mbali na kufungua ubalozi wake huko Tel Aviv Imarati imechangamkia pia suala la kuwakaribisha nchini humo viongozi wa utawala ghasibu wa Israel akiwemo Rais Yitzhak Herzog.
Wakati huo huo, mbali na kuzishawishi nchi nyingine za Kiarabu zianzishe uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, Imarati imekuwa mstari wa mbele katika kuandaa vikao vinavyowashirikisha watawala wa Kizayuni na wa nchi za Kiaraba ambazo tayari zina uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo. Kuhusiana na hilo, Imarati imehudhuria mkutano wa Sharm el-Sheikh huko Misri na vile vile mkutano wa Jangwa la Naqab huko Israel. Madai ya Imarati katika uwanja huo ni kuwa suala hilo litaleta amani katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kati ya Wazayuni na Wapalestina.
Pamoja na hayo, vita vya siku 11 vilivyojiri mwaka uliopita, mashambulio ya kila uchao ya utawala wa kibaguzi wa Israel na vitendo vya mabavu vinavyofanywa na utawala huo dhidi ya Wapalestina katika maeneo tofauti ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na za Wapalestina, vinathibitisha wazi kwamba mitazamo ya nchi kama vile Imarati kuhusu utawala wa kigaidi wa Israel si tu haitaleta amani yoyote katika eneo la Mashariki ya Kati bali inaandaa mazingira ya utawala huo kuongeza mashinikizo na ukatili wake dhidi ya Wapalestina.
Kuhusu hilo, tangu mwanzo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani hadi sasa Wapalestina wasiopungua 17 wameuawa shahidi na askari wa utawala wa Israel ambapo vitendo vyao vya mabavu na ugaidi vimefikia kilele katika maeneo mengi ya Wapalestina hasa huko Jenin, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Ijumaa iliyopita, askari-jeshi wa Israel waliwashambulia Wapalestina waliokuwa wakitekeleza ibada zao katika Msikiti wa al-Aqswa ambapo waliwatia nguvuni watu 400 na kuwajeruhi wengine 450. Licha ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Imarati kulaani kitendo hicho lakini ni wazi kuwa hatua kama hizo za kidhahiri tu zinachukuliwa kwa malengo ya kisiasa na serikali ya Imarati kivitendo inatekeleza siasa tofauti ambazo zinaenda kinyume na matamshi hayo yanayolenga kuwatuliza Waislamu na Waarabu kuhusu kadhia hiyo. Imarati imechukua hatua mbili muhimu dhidi ya Wapalestina katika uwanja huo.
Hatua ya kwanza ni kukubali ujenzi wa kitongiji kitakachowapa makazi Mayahudi wapatao 8000 huko Imarati. Kwa sasa Mayahudi 2500 wanaishi Imarati na Kuhani Eli Ebadi, Mkuu wa Jumuiya za Mayahudi katika Ghuba ya Uajemi ametabiri kwamba idadi hiyo ya Mayuhudi itaongezeka mara 4 zaidi katika miaka mitano ijayo.
Hatua ya pili ni uamuzi wa Imarati kushiriki kwenye sherehe za maadhimisho ya 74 ya kuasisiwa utawala haramu wa Israel ambazo zimepangwa kufanyika tarehe 15 mwezi Mei ujao. Wapalestina wanaichukulia siku hiyo kuwa Siku ya Maafa Makubwa kwao na sasa Imarati imeamua kushiriki kwenye sherehe hizo katika siku hiyo ya huzuni kwa taifa la Palestina ili kutoa pigo jingine kubwa kwa malengo na maslahi ya Wapalestina.
Hatua zote mbili hizo zinathibitisha wazi kwamba Imarati imeazimia kufumbia macho na kuvuka mistari yote miwili myekundu ya Uarabu na Usialmu katika siasa zake za nje na kucheza katika uwanja wa utawala wa kibaguzi wa Israel. Katika upande wa pili uamuzi huo unaonyesha kuwa serikali ya Abu Dhabi haijali na imeamua kufumbia macho jinai na ugaidi wote unaotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia, kinyume kabisa na sheria za kimataifa.