Hamas yautahadharisha utawala haramu wa Israel: Usicheze na moto
-
Abdul Latif al-Qanoo
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetahadharisha kuhusu vitendo vya kichochezi vya Wazayuni katika Msikiti wa Al-Aqsa na kusema vitendo hivyo ni sawa na kucheza na moto.
Alkhamisi ya leo Wazayuni wamepanga kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa wakiwa na bendera ya utawala ghasibu wa Israel kwa mnasaba wa kile kinachoitwa siku ya uhuru wa utawala huo, na kuimba wimbo wa utawala haramu ndani ya msikiti huo mtakatifu.
Polisi wa utawala wa Kizayuni pia wamekubali rasmi kuruhusu hujuma ya walowezi wa Kiyahudi katika Msikiti wa Al-Aqsa leo Alhamisi kwa ajili ya shughuli hiyo.
Kufuatia hatua hiyo, harakati ya Hamas imetoa taarifa na kutangaza kuwa, hujuma yoyote dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa italielekeza eneo la Magharibi mwa Asia katika hali ambayo baraza la mawaziri la Israel ndilo litakalobeba dhima ya kuhusika nayo.
Hamas imewataka Wapalestina shujaa kuhudhuria kwa wingi katika Msikiti wa al Aqsa na kuwa tayari kulinda utambulisho, dini na kibla chao cha kwanza.
Msemaji wa Hamas, Abdul Latif al-Qanoo amesema: Idhini ya polisi ya utawala wa Kizayuni ya kuwaruhusu walowezi wa Kiyahudi kuvamia Msikiti wa Al-Aqsa siku ya Alkhamisi ya leo itakuwa cheche ya kuanzisha vita vingine na adui Mzayuni.
Al-Qanoo amesisitiza kuwa, wananchi wa Palestina kamwe hawatawaruhusu Wazayuni kukariri vitendo vya kuuvunjia heshima na kuushambulia Msikiti wa Al-Aqsa.
Msikiti wa Al-Aqsa ambao ni nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Palestina wa mji wa Quds (Jerusalem), daima umekuwa ukilengwa kwa vitendo vya uharibifu vya utawala haramu wa Israel na walowezi wa Kizayuni.