Ziyad al-Nakhalah: Adui Mzayuni anaelekea kuangamia
Ziyad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amesema kuuwa, adui Mzayuni anaelekea kuangamia.
Ziyad al-Nakhalah amesisitiza kuwa, mujahidina wa Kipalestina hawapaswi kuwa na shaka wala kigugumizi katika vita na adui Mzayuni kwani adui huyo muda si mrefu ataangamia.
Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina ameongeza kuwa, wananchi wa Palestina ni wadaiwa wa damu ya mashahidi kwani wamekuwa wakikabiliana na utawala wa muda wa Israel tangu ulipoasisiwa katika ardhi za Palestina.
Aidha amesema kuwa, lengo la utawala wa Kizayuni wa Israel ni kuwashinda wananchi wa Palestina kupitiai mauaji, hivyo la msingi ni Wapalestina kusimama kidete kwa kuendeleza mapambano ya muqawama dhidi ya adui huyu asiyefahamu lugha nyingine ghairi ya vita.
Kiongozi huyo wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amewataka Wapalestina kuelekeza silaha zao upande wa adui na kuzitumia kwa wakati na eneo mwafaka.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel Ehud Barak alisema kuwa, ana wasiwasi mkubwa kuwa yamkini utawala huo utaangamia kabla ya kuadhimisha mwaka wa 80 tokea uasisiwe.
Mwaka huu utawala bandia wa Israel umeadhimisha mwaka wa 74 tokea uasisiwe katika ardhi ya Wapalestina. Ikumbukwe kuwa mwezi Mei mwaka 1948, utawala bandia wa Israel ulitangaza uwepo wake baada ya kufanya mauaji makubwa ya umati dhidi ya Wapalestina.