Lebanon yakamilisha maandalizi ya uchaguzi wa Bunge, unafanyika kesho
Waziri Mkuu wa Lebanon amesema kuwa, nchi hiyo imefanya maandalizi yote yanayohitajika kwa ajili ya uchaguzi wa Bunge nchini humo.
Uchaguzi wa wabunge wa Lebanon utafanyika kesho ndani ya nchi kuwachagua wawakilishi 128.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Waziri Mkuu wa Lebanon, Najib Mikati amesema wakati wa mkutano na ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya mjini Beirut kwamba serikali ya Lebanon imefanya mipango yote muhimu kwa ajili ya kuitisha uchaguzi huru na wa kidemokrasia wa bunge.
Mikati pia amejibu tuhuma za ukiukwaji wa taratibu katika uchaguzi huo wa Bunge, akisema kuwa pamoja na kwamba madai hayo yanatolewa katika chaguzi zote, mamlaka husika inachunguza suala hilo.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Lebanon Bassam Rumi ametia saini hati ya makubaliano na ujumbe wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwa ajili ya kusimamia zoezi la uchaguzi wa Bunge la Lebanon.
Vilevile ubalozi wa Russia mjini Beirut ulitangaza jana kuwa kundi la waangalizi wa nchi hiyo limeelekea Beirut kwa ombi la Lebanon kwa ajili ya kufuatilia uchaguzi wa Bunge la nchi hiyo.