HAMAS: "Maandamano ya Bendera" yasipoghairishwa yamkini tukatoa jibu kwa kombora
Kiongozi mmoja mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, "ikiwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel hautaacha uvamizi wake dhidi ya msikiti wa Al Aqsa na hautaghairisha maandamano ya bendera, katika hali hiyo tutafikisha ujumbe wetu kwa kombora."
Mushir al Masri amesisitiza kuwa, hakuna shaka yoyote kwamba maandamano ya bendera ambayo adui Mzayuni anataka kuyafanya ni ukiukaji wa mistari yote myekundu.
Al Masri ameongeza kuwa "tunamhadharisha adui Mzayuni na mpango huu wa kuchezea moto na tunatangaza kuwa muqawama umejiweka tayari kikamilifu na silaha mkononi, ukiongojea kupewa ishara tu."
Kiongozi huyo mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina amesisitiza kwa kusema, viongozi wa adui wanapaswa kufikiria upya suala la kuitisha maandamano ya bendera kabla hawajautoa mhanga mustakabali wao wa kisiasa kwa suala hilo; na akaongezea kwa kusema: "Ninawaasa wasirudie kuujaribu tena muqawama."
Maandamano ya bendera ya utawala wa Kizayuni hufanyika tarehe 10 Mei kila mwaka kwa mnasaba wa kuanza kukaliwa kwa mabavu na Wazayuni eneo la kale la mji mtukufu wa Baytul Muqaddas.
Wazayuni wanadai eti mji wa Quds ndio mji mkuu wa utawala huo pandikizi. Lakini wananchi wa Palestina wanasema , Quds ndio mji mkuu wa nchi ya Palestina na kwamba upotoshaji wowote ule hauwezi kufifiliza wala kusahaulisha uhakika huo.../