Naftali Bennett akiri: Israel inakaribia kusambaratika
Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Naftali Bennett, ameashiria fujo na mchafukoge unaoshuhudiwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kukiri kuwa Israel inakaribia zaidi kusambaratika.
Wasiwasi wa kusambaratika utawala wa Kizayuni umewapata maafisa wengi wa usalama na intelijensia wa utawala huo; na baadhi yao wametahadharisha kuhusu suala hilo katika minasaba tofauti.
Katika ujumbe aliowatumia walowezi wa Kizayuni, Bennett amesema, "Israel inakabiliana na mtihani hasa, na tunashuhudia hali ambayo haijawahi kushuhudiwa inayokaribia kwenye msambaratiko na inayokabiliana na njiapanda ya kihistoria."
Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Kizayuni ameashiria machafukoge, chaguzi za mara kwa mara pamoja na kuvunjika kwa serikali zilizoundwa katika miaka iliyopita katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na akasema, "utawala huu umefikia kwenye moja ya vipindi vigumu zaidi vya mkengeuko".
Hadi sasa maafisa kadhaa wa kisiasa, kiusalama na kijeshi pamoja na shakhsia wa kiakademia na wa vyombo vya habari vya Kizayuni wamezungumzia uwezekano wa kuporomoka na kusambaratika utawala haramu wa Israel.
Ari Shavit, mchambuzi wa Kiyahudi wa gazeti la Kiebrabia la Haaretz ameeleza katika makala ya uchambuzi aliyoandika kwa anuani: 'Israel inavuta pumzi zake za mwisho' ya kwamba: "hakuna mahali tena pa kuishi ndani ya Iisrael na inapasa tuondoke hapa".../