Lebanon yaionya vikali Israel, vita vyanukia katika Bahari ya Mediterania
Rais wa Lebanon Michel Aoun ameuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba usijaribu kuchimba gesi katika Bahari ya Mediterania kabala ya mgogoro wa mpaka wa baharini baina ya pande mbili kutatuliwa.
Rais Aoun amesema hatua yoyote ya Israel ya kuchimba gesi kabla ya kusuluhishwa mzozo itaonekana kama ni uchokozi jambo ambalo linaashiria uwezekano wa kuzuka vita baina ya pande hizo mbili katika maji ya Mediterania yenye utajiri mkubwa wa gesi asilia.
"Kitendo au shughuli yoyote katika eneo linalozozaniwa ni sawa na uchochezi na ni kitendo cha kichokozi," Aoun alisema Jumapili katika taarifa.
Rais wa Lebanon ametoa kauli hiyo baada ya meli ya kuhifadhi na kubeba gesi (FPSO) kufika katika eneo linalozozaniwa, ambapo kampuni yenye makao yake makuu London ya Energean inapanga kuanza kuvuta gesi kutoka chini ya bahari katika eneo la Karish chini ya mkataba na utawala wa Kizayuni wa Israeli baadaye mwaka huu.
Aoun amesema amejadili kuwasili kwa meli hiyo na Waziri Mkuu Najib Mikati na kumtaka Kamanda wa Jeshi la Lebanon kumpa "data sahihi na rasmi kuhusu suala hilo."
Mikati ameitaja hali hiyo kuwa "hatari sana," akisema Israel ilikuwa inajaribu "kuzua mgogoro mpya, kuingilia utajiri wa bahari wa Lebanon na kulazimisha misimamo yake katika eneo linalozozaniwa."
Eneo la Karish liko karibu kilomita 90 magharibi mwa mji wa Haifa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel, karibu na maeneo yenye hifadhi nyingi zaidi ya gesi ya Leviathan na Tamari. Energean ilitia saini mkataba mwezi Machi wa kuuza gesi kutoka Karish kwa shirika la utawala haramu wa Israel la Electric Co., mnunuzi mkubwa wa gesi katika utawala huo.
Utawala haramu wa Israel umedai kuwa Karish iko katika ukanda wake Maalum wa Kiuchumi (EEZ), lakini Rais Aoun amesema mazungumzo ya kusuluhisha suala hilo yanaendelea, na pande zote mbili zimewasilisha malalamiko kwa Umoja wa Mataifa kuhusu umiliki wa eneo hilo la baharini.
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imewahi kuonya kuwa itachukua hatua iwapo utawala ghasibu wa Israel utachimba mafuta au gesi katika eneo linalozozaniwa kabla ya suluhisho kupatikana.