Hizbullah: Muqawama ni udharura wa kimkakati wa kumkwamisha adui
Mjumbe mmoja wa Baraza Kuu la Hizbullah ya Lebanon amelaumu baadhi ya mirengo inayoshirikiana na Marekani ndani ya Lebanon na kusisitiza kuwa, muqawama na mapambano ni udharura wa kimkakati wa kumkwamisha adui kwenye kinamasi na kumzuia asifikirie kabisa kushambulia ardhi ya Lebanon.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Sheikh Nabil Qawuq alisema hayo jana na kuongeza kuwa, Marekani inafanya njama za kuikwamisha Lebanon kiuchumi na kifedha ili kuilazimisha ikubaliane na matakwa ya utawala wa Kizayuni, hivyo haifai kabisa kuilegezea kamba hata kidogo Marekani.
Ikumbukwe kuwa, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinauona muqawama kuwa ni tishio kubwa kwao na ndio maana zinamwaga fedha kwa asasi za kiraia ili kudhoofisha mori wa wananchi wa Lebanon, kuwafanya wachukie muqawama wa nchi yao na vile vile kutaka wasiiunge mkono Hizbullah kila inaposimama imara kujibu jinai za utawala wa Kizayuni.
Sheikh Qawuq pia amesema, mgogoro wa hivi sasa wa Lebanon unatokana na baadhi ya watu na vyama kujisalimisha kwa Marekani na kusisitiza kuwa, kadiri baadhi ya watu wanavyoendelea na siasa zao za kuibebembeleza Marekani, kuomba msaada kwake na kujidhalilisha mbele ya dola hilo la kibeberu, ndivyo hatari ya kusambaratika Lebanon inavyozidi kuwa kubwa.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah, amesisitiza pia kuwa, baada ya uchaguzi wa Bunge, kumejitokeza fursa nzuri ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo kupitia mazungumzo na maelewano baina ya wananchi wenyewe wa Lebanon bila ya kuruhusu uingiliaji wa madola ya nje.