Umoja wa Mataifa: Hali ya Gaza ni janga na maafa matupu
Ripoti iliyotolewa jana Ijumaa na Umoja wa Mataifa imeitaja hali ya sasa katika eneo la Ukanda wa Gaza kuwa ni janga tupu.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ilisema katika ripoti yake kuwa, kuzingirwa Ukanda wa Gaza kumeongeza hali ya umaskini na ukosefu wa ajira katika eneo hilo, kuharibu uchumi wa Wapalestina, na kuwafanya asilimia 50 miongoni mwao wategemee misaada ya kimataifa.
OCHA pia imesema katika ripoti yake kwamba kuzingirwa kwa ukanda wa Gaza kumepelekea kufa shahidi mamia ya wakaazi wa ukanda huo.
Katika ripoti hiyo, OCHA imesisitiza ulazima wa kuondoa mzingiro wa Isarel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza kwa mujibu wa Azimio nambari 1860 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu katika Maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, hali katika Ukanda wa Gaza imekuwa mbaya baada ya miaka 16 ya kuzingirwa kwa ardhi, bahari na anga katika eneo hili.
Umoja wa Mataifa hapo awali ulikuwa umesema kuwa Ukanda wa Gaza unakabiliwa na janga la binadamu na kutangaza kuwa eneo hilo si mahali pa kuishi tena.
Mzingiro wa Ukanda wa Gaza unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa miaka kadhaa umesababisha upungufu wa chakula na ongezeko la watu wenye njaa katika eneo hilo, kiasi ambacho Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeeleza wasiwasi wake kuhusu jambo hilo katika ripoti zake.