Kadhia ya Palestina ndicho kipaumbele muhimu zaidi kwa Waislamu wa Marekani
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa nchini Marekani yanaonyesha kuwa Waislamu wengi wa nchi hiyo wanalichukulia suala la Palestina kuwa ndicho kipaumbele kikuu kwao.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu CAIR, katika mambo yanayozishughulisha fikra za Waislamu wa Marekani kwa upande wa masuala ya kimataifa, kadhia ya Palestina ina nafasi ya juu zaidi; na wakati huohuo nusu ya jamii ya Waislamu wa Marekani hawakubaliani na sera za serikali ya sasa ya nchi hiyo.
Matokeo hayo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu yanaonyesha pia kuwa sehemu kubwa ya jamii ya Waislamu waliotimiza masharti ya kupiga kura hawaridhiki na utendaji wa rais wa nchi hiyo Joe Biden; lakini kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni Waislamu haohao wanafadhilisha kuwapigia kura wagombea wa chama cha Democratic kuliko wale wa Republican katika uchaguzi wa bunge wa katikati ya muhula wa urais ambao utafanyika mwezi Novemba mwaka huu.
Kwa muda wa miaka mitatu sasa, Palestina imekuwa katika hali mbaya kifedha kutokana na kuzuiliwa fedha zake zinazotokana na kodi zinazokusanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kupungua misaada inayopokea kutoka nje.
Ili kuhakikisha unafikia malengo yake ya kujipanua, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, kila siku unavamia maeneo mbalimbali ya Palestina na kuwaua shahidi, kuwajeruhi au kuwakamata na kuwaweka gerezani Wapalestina.
Katika miezi ya karibuni, jinai za askari na walowezi wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina zimeongezeka kwa kiwango kikubwa katika pande tofauti; na kutokana na jinai hizo makumi ya Wapalestina wameuawa shahidi na mamia ya wengine wamejeruhiwa.../