Shambulio la Saudia nchini Yemen laua na kujeruhi mamia ya watu
Muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kwa mara nyingine umekiuka makubaliano ya usitishaji wa Umoja wa Mataifa, na kuua na kujeruhi mamia ya raia wa Yemen katika shambulio jipya, kaskazini mwa nchi.
Tovuti ya shirika la habari la Saba la Yemen imeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, Wayemen 31 wameuawa huku wengine zaidi ya 260 wakijeruhiwa, baada ya vikosi vya muugano wa Saudia kushambulia maeneo ya mipakani ya mkoa wa Sa’ada, wa kaskazini magharibi mwa nchi.
Duru za habari zimeripoti kuwa, aghalabu ya Wayemen waliojeruhiwa kwenye hujuma hiyo ya jana Jumapili wanatibiwa katika hospitali ya mji wa Razih, magharibi mwa mkoa huo.
Habari zaidi zinasema kuwa, baadhi ya majeruhiwa hao wapo katika hali mbaya, na yumkini idadi ya wahanga wa shambulio hilo ikaongezeka.
Inaarifiwa kuwa, mtu mmoja ameuawa huku wengine saba wakijeruhiwa, katika shambulio jingine la wanajeshi hao vamizi wa muungano wa Saudia, katika wilaya ya Shada’a mkoani hapo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Yemen, utawala wa kifalme wa Saudia ambao uliivamia Yemen mwaka 2015 ikisaidiwa na Marekani na washirika wake wa Kimagharibi na Kiarabu, umeua Wayemen 387, huku ukipuuza usitishaji vita wa UN ulioanza kutekelezwa mnamo Aprili 2.