UN yalaani kufungwa jela miaka 34 mwanaharakati mwanamke Saudia
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limekosoa hatua ya watawala wa Saudi Arabia ya kumpa hukumu nzito mwanaharakati mwanamke kutokana na ujumbe wake wa Twitter.
Taarifa ya baraza hilo la UN imesema, hukumu dhidi ya mtetezi huyo wa haki za binadamu ndiyo ya muda mrefu zaidi dhidi ya mwanaharakati wa kike nchini humo.
Siku chache zilizopita, utawala wa Aal-Saud ulimhukumu mwanamke huyo kwa jina Salma al-Shehab, 34, kifungo cha miaka 34 jela, eti kwa kupatikana na hatia ya kumiliki ukurasa wa Twitter na kusambaza ujumbe unaoukosoa utawala wa Aal-Saud kupitia mtandao huo wa kijamii.
Mama huyo wa watoto wawili na pia mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza alikamatwa na vyombo vya usalama vya Saudia Januari mwaka jana, alipokuwa amejerea nyumbani kwa ajili ya likizo. Awali alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 6 jela, kwa kupatikana na hatia ya eti 'kutumia mitandao ya kijamii kuvuruga nidhamu ya umma na kuhatarisha usalama na uthabiti wa dola.'
Hata hivyo Mahakama ya Rufaa imeangalia upya hukumu hiyo na kumsweka jela miaka 34, mbali na kumpiga marufuku ya kusafiri nje ya nchi kwa kipindi cha miaka 34.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiongozwa na Human Rights Foundation, Freedom Initiative, European Saudi Organization for Human Rights (ESOHR) na ALQST for Human Rights yamelaani hukumu hiyo, na kusema ni muendelezo wa wimbi la ukandamizaji na mbinyo unaofanywa na utawala wa Riyadh ukiongozwa na Mohammed bin Salman, Mrithi wa Ufalme wa Saudia, dhidi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii, wanaharakati na wakosoaji wa utawala huo wa kifalme.