Jun 10, 2016 03:49 UTC
  • Iraq: Daesh inatega mabomu ndani ya nakala za Qur'ani

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh linatumia nakala za Qur'ani tukufu kutekeleza mashambulizi yake ya mabomu katika mji wa Fallujah nchini Iraq.

Ibrahim al-Jafari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq ameliambia shirika la habari la al-Ghad al-Arabi kuwa, wanachama wa Daesh wameanza kutega mabomu ndani ya nakala za Qur'ani Tukufu katika mbinu mpya ya kutekeleza hujuma dhidi ya askari wa Iraq katika mji wa Fallujah. Al-Jafari amesema kuwa, mbinu hiyo ya kukidhalilisha kitabu kitufuku cha Uislamu ni dhihirisho tosha kuwa kundi hilo la kigaidi halijui wala kuheshimu mafundisho sahihi ya dini hiyo tukufu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq ameongeza kuwa, mbinu hii ya Daesh kutega mabomu ndani ya nakala za Qur'ani haitakua na tija nyingine ghairi ya kuwapa nguvu na motisha askari wa Iraq ambao wanazidi kupata mafanikio makubwa katika mji wa Fallujah.

Hapo jana (Alkhamisi), kundi la Daesh lilifanya mashambulio mawili ya bomu ya ulipizaji kisasi, kufuatia operesheni za jeshi la Iraq kwa kushirikiana na harakati za kujitolea za wananchi 'Hashdu ash-Shabi' kupata mafanikio makubwa katika operesheni za kuukomboa mji wa kistratijia wa Fallujah mkoani al-Anbar, magharibi mwa nchi hiyo.

Tags