Iraq yapinga tena uingiliaji wa Saudia na Uturuki nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i9055-iraq_yapinga_tena_uingiliaji_wa_saudia_na_uturuki_nchini_humo
Serikali ya Iraq imelalamikia hatua ya watawala wa Saudi Arabia ya kukusanya misaada ya kifedha kwa ajili ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2016 09:38 UTC
  • Iraq yapinga tena uingiliaji wa Saudia na Uturuki nchini humo

Serikali ya Iraq imelalamikia hatua ya watawala wa Saudi Arabia ya kukusanya misaada ya kifedha kwa ajili ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.

Katika radiamali yake Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq, imeitaka Riyadh kulitolea ufafanuzi suala lenye kushadidisha mvutano la baadhi ya makundi ya nchi hio kukusanya misaada ya kifedha kwa ajili ya magaidi wanaotenda jinai dhidi ya binaadamu huko nchini Iraq. Hatua hiyo imekuja baada ya kukiri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia kuwa kufahamu fika suala hilo. Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq pia imeitaka Saudia kuacha mara moja kutoa matamshi yasiyofaa dhidi ya harakati ya kujitolea ya wananchi ya 'Hashdu sh-Shaabi' ambayo ni sehemu ya jeshi la nchi hiyo. Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema kuwa, kitendo cha kukusanya misaada ya kifedha kwa ajili ya kundi la kitakfiri la Daesh ndani ya ardhi ya Saudia, ni kwenda kinyume na maamizimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kabla ya hapo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia ilitangaza kuwa, inao uwezo wa kukabiliana na harakati za ukusanyaji misaada ya kifedha ya wananchi kwa ajili ya kundi la Daesh (ISIS), lakini haifanyi hivyo kwa kuwa suala hilo eti linahusiana na wananchi wenyewe. Mansour Al-Turki, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia aliongeza kuwa, ushiriki wa harakati ya kujitolea ya wananchi nchini Iraq 'Hashdu sh-Shaabi' kwa ajili ya kuukomboa mji wa Fallujah, ndio iliyowafanya wananchi wa Saudia kukusanya misaada ya kifedha kwa ajili ya genge hilo la kigaidi. Ukweli ni kwamba, maadui wa taifa la Iraq hususan Saudia, hivi sasa wanafanya njama kubwa kupitia propaganda zao chafu kwa ajili ya kuibua tofauti baina ya jeshi la Iraq na harakati hiyo ya kujitolea ya wananchi. Vyombo vya habari vya Saudia na kwa kisingizio cha ushiriki wa harakati hiyo ya wananchi ya 'Hashdu sh-Shaabi' katika kuukomboa mji wa Fallujah, vinajaribu kuonyesha kuwa, vita vya kuukomboa mji huo ni vita vya kimadhehebu baina ya Suni na Shia ili kwa njia hiyo vyombo hivyo viweze kuchochea raia wa mataifa ya Kiarabu wakusanye misaada zaidi ya kifedha na kuwapelekea magaidi wa Daesh maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu na ambao hivi sasa wanaelekea kushindwa. Wawakilishi wa bunge la Iraq pia wamemtaja balozi wa Saudia mjini Baghdad, kuwa muhusika mkuu katika kuibua tofauti nchini Iraq. Mowaffak al-Rubaie, mwakilishi wa bunge la Iraq na mshauri wa zamani wa masuala ya usalama wa ndani nchini humo, sanjari na kuashiria mafanikio ya operesheni za kuukomboa mji wa Fallujah, amekosoa pia matamshi ya kichochezi ya balozi huyo. Al-Rubaie ameongeza kuwa, ugaidi utaendelea madamu wataendelea kuwepo watu wenye fikra za Kiwahabi wanaounga mkono kisilaha na kilojestiki makundi hayo ya kigaidi. Hii ni katika hali ambayo baada ya ushindi mkubwa wa harakati ya kujitolea ya wananchi nchini Iraq katika mkoa wa Salah ad Din na al-Anbar sanjari na kukombolewa mji wa kistratijia wa Tikrit na miji mingine muhimu ya Iraq kutoka mikononi mwa Daesh, vyombo vingi vya habari vya nchi za Kiarabu hususan katika nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi vilishadidisha hujuma ya kuchafua sura halisi ya harakati za wananchi na jeshi la nchi hiyo. Wakati huo huo, uingiliaji wa Uturuki na hatua yake ya kukiuka haki ya kujitawala Iraq, imekabiliwa na radiamali kali za Wairaki. Katika uwanja huo, mwakilishi wa mkoa wa Nainawa katika bunge la Iraq, amelaani vikali kuendelea kuwepo askari wa Uturuki katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo. Abdulrahman al-Luwaiz aliyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la al-Maalumah ambapo sanjari na kuonya hatua ya uepo wa askari wa Uturuki eneo la Bashiqa karibu na mji wa Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa, amekitaja kitendo hicho kuwa ni hatari kuliko hata uepo wa wapiganaji wa kundi la ukufurishaji la Daesh. Itakumbukwa kuwa, makumi ya askari wa Uturuki waliingia eneo hilo mwezi Disemba mwaka jana kwa kisingizio cha kukabiliana na wapiganaji wa Kikurdi wa Peshmerga. Hii ni katika hali ambayo serikali ya Iraq imekuwa ikiitaja hatua hiyo kuwa ni ukiukaji wa wazi wa haki ya kujitawala taifa la Iraq, huku ikisisitizia umuhimu wa kuondoka askari hao vamizi wa Uturuki katika eneo hilo.