Mussa Abu Marzouq: Israel itasambaratika endapo Wamagharibi wataacha kuiunga mkono
Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, endapo madola ya Magharibi yatasitisha himaya na uungaji mkono wao kwa utawala haramu wa Israel basi siku itakayofuata utawala huo utasambaratika kikamilifu.
Mussa Abu Marzouq ameeleza kuwa, madola ya Magharibi yanaunga mkono mpango wa utawala ghasibu wa Israel katika eneo la Asia Magharibi na yanausaidia utawala huo bandia huku yakiupatia kila msaada kuhakikisha kuwa unabakia hai.
Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameongeza kusema kuwa, mazingira ya sasa ambayo inayo malengo matukufu ya Palestina katika upande wa taathira ya kisiasa na mchango wake katika uga wa kimataiifa ni bora ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesifu misimamo ya Algeria kuhusiana na kadhia ya Palestina na kueleza kwamba, nchi hiyo ni imara na inaweza kubeba jukumu la kuleta maridhiano ya Palestina na kubeba mzigo wa mapinduzii ya Palestina.
Sambamba na kutilia mkazo kuhusu fursa kubwa iliyoko mbele ya Wapalestina ya kusimama na kutumia nguvu zao zote kwa ajili ya Intifadha mpya, Mussa Abu Marzouq amebainisha kwamba, Palestina inaweza kuwaamsha watu wake kwa sharti kwamba, Mamlaka ya Ndani ya Palestina isiwe na ndoto za kuzisaliti ardhi za Palestina.
Madola ya Magharibi hususan Marekani ni waungaji mkono wakuu wa jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika eneo la Asia Magharibi na hata yamekuwa yakiushajiisha utawala huo vamizi uendelee kufanya mauaji na jinai dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.