HAMAS: Muqawama ndiyo njia pekee ya kupambana na magaidi Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i91494-hamas_muqawama_ndiyo_njia_pekee_ya_kupambana_na_magaidi_wazayuni
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kuwa, muqawama ndiyo njia na chaguo poekee la taifa la Palestina katika kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 09, 2022 06:59 UTC
  • HAMAS: Muqawama ndiyo njia pekee ya kupambana na magaidi Wazayuni

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kuwa, muqawama ndiyo njia na chaguo poekee la taifa la Palestina katika kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tamko hilo la HAMAS limetolewa baada ya wanajeshi magaidi na makatili wa Israel kumuua kidhulma kijana mwingine mmoja wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Jana Alkhamisi, wanajeshi madhalimu wa utawala wa Kizayuni walimuua kigaidi kwa kumpiga risasi, kijana wa miaka 17 wa Kipalestina anayejulikana kwa jina la Diaa (Dhwiyaau) Muhammad Shafiq al Rimawi karibu na kijiji cha Abud, kaskazini magharibi mwa Ramadhallah.

Vyombo vya habari vya Palestina vimenukuu taarifa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu HAMAS ikitoa mkono wa pole kwa kuuawa shahidi kijana huyo na kusema kuwa, muqawama wa pande zote ndilo chaguo pekee lililobakia la taifa la Palestina katika kupambana na wavamizi wa Quds na adui Mzayuni ambaye lazima atabeba dhima ya yote yatakayotokea baada ya kumuua kidhulma kijana huyo mdogo wa Kipalestina. 

Diaa Muhammad Shafiq al Rimawi, kijana mdogo wa Kipalestina aliyepigwa risasi na kuuliwa shahidi na wanajeshi wa Israel jana Alkhamisi huko Ramadhallah

 

Hamas pia imesema, damu za Wapalestina zinazomwagwa na Wazayuni ikiwemo ya kijana al Rimawi na wakazi wa Jenin, hazitoachwa kumwagika hivi hivi bila ya majibu makali.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS aidha imesema, tuko pamoja na vijana wanamapinduzi wa Kipalestina na tutahakikisha mapambano dhidi ya adui na walowezi wa Kizayuni yanaendelea hadi ardhi zote za Palestina zitakapokombolewa. 

Alfajiri ya jana Alkhamisi pia, vijana watatu wa Palestina waliuliwa shahidi na wanajeshi makatili wa Israel wakati wanajeshi hao walipoivamia kambi ya Jenin, ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.