Netanyahu: Azimio la UN dhidi ya Israel halina umuhimu, linakirihisha
(last modified Sun, 01 Jan 2023 07:24:33 GMT )
Jan 01, 2023 07:24 UTC
  • Netanyahu: Azimio la UN dhidi ya Israel halina umuhimu, linakirihisha

Waziri Mkuu wa Israel amesema azimio jipya lililopitishwa dhidi ya utawala huo haramu katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa halina maana wala umuhimu wowote.

Benjamin Netanyahu alisema hayo jana Jumamosi na kueleza kuwa, hatua ya Baraza Kuu la UN ya kupiga kura dhidi ya utawala huo wa Kizayuni inachukiza na kukirihisha.

Netanyahu ambaye karibuni alipata kura ya kuwa na imani naye kwenye bunge la utawala haramu wa Israel (Knsset) na hivyo kupata fursa nyingine ya kuongoza baraza la mawaziri la utawala huo amesema Tel Aviv haitofungamana na azimio hilo la UN. 

Juzi Ijumaa, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura ya kuunga mkono mpango uliowasilishwa na Palestina, kuhusiana na kutolewa uamuzi wa kisheria na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC iliyoko The Hague kuhusu asili na hali ya kisheria uliyonayo utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel katika ardhi ya Palestina.

Azimio hilo lilipasishwa kwa kupigiwa kura ya 'Ndiyo' na nchi 86, huku nchi 26 pekee ikiwemo Marekani, DRC, Uingereza, Ujerumani na Italia zikilipigia kura ya 'Hapana'.

Kikao cha Baraza Kuu la UN

Haya yakijiri katika hali ambayo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imeukosoa Umoja wa Mataifa kwa kupitisha maazimio kadhaa likiwemo la juzi Ijumaa dhidi ya utawala wa Kizayuni bila ya kufikiria njia za kivitendo za kuwezesha utekelezaji wake.

Hata hivyo Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa taarifa ya kupongeza kupasishwa kwa azimio hilo la Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni ikisisitiza kuwa, itaendelea kuunga mkono kadhia ya Palestina kwa kuzingatia sheria za kimataifa.

Aidha viongozi wa Wapalestina wamepongeza kupasishwa azimio hilo wakieleza kuwa, kura ya 'Ndiyo' ya UN kwa azimio hilo ni ishara ya uungaji mkono wa walimwengu kwa watu wa Palestina na haki zao za kihistoria.