Sababu za umuhimu wa safari ya Amir-Abdollahian nchini Lebanon
Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kuzungumza na Abdallah Bou Habib, Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Lebanon katika safari yake mjini Beirut na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima itaendelea kuwa rafiki mwaminifu na wa kutegemewa wa Lebanon.
Hii ni safari ya tatu ya Amirabdollahian nchini Lebanon akiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran. Lebanon ni moja ya nchi ambazo zina nafasi maalumu katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Iran ni muungaji mkono mkubwa zaidi wa mrengo wa mapambano wa Lebanon katika vita vyake dhidi ya utawala haramu wa Israel na inasisitiza juu ya kuendeleza uungaji mkono huo kwa taifa la Lebanon.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima inataka kudumishwa amani na utulivu huko Lebanon na huku ikijiepusha kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo imeyasihi na kuyashawishi makundi yote ya kisiasa na kijamii kufanya kila linalowezekana kwa ajili ya kubuni serikali moja yenye nguvu. Suala hilo pia limesisitizwa mara hii na Amirabdollahian katika mazungumzo yake na waziri mwenzake wa Lebanon, Abdallah Bou Habib.
Katika uwanja huo, Hossein Amirabdollahian, amesisitiza uungaji mkono wa Jamuri ya Kiislamu ya Iran kwa juhudi zozote za kuimarisha uthabiti na utulivu wa Lebanon na kuongeza kuwa Iran haitaingilia kwa vyo vyote vile masuala ya ndani ya nchi hiyo rafiki na ndugu na kwamba itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na makundi yote ya kisiasa ya nchi hiyo kwa lengo la kufikia muwafaka wa kisiasa kwa ajili ya kubuniwa serikali yenye nguvu itakayolinda maslahi ya watu wa Lebanon. Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba Abdallah Bou Habib pia ametambua na kuisifu Iran kutokana na uungaji mkono na mchango wake katika kuimarisha uthabiti na usalama wa Lebanon na pia nia ya Tehran ya kuyasaidia makundi ya nchi hiyo kutatua matatiso yake ya kisiasa na kiuchumi.
Mbali na hayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa tayari kuisaidia Lebanon katika mazingira mahumu kabisa, katika hali ambayo nchi za eneo na kimataifa ambazo hutoa madai ya uongo ya eti kuwasaidia Walebanon si tu zimekuwa zikikaa pembeni na kutofanya lolote kwa ajili ya kupunguza mizozo na matatizo ya watu wa nchi hiyo bali hata zimekuwa zikichochea zaidi matatizo ya ndani ya nchi hiyo. Moja ya sababu za mgogoro wa hivi sasa wa kiuchumi wa Lebanon ni vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na kukatwa misaada ya kieneo dhidi ya nchi hiyo. Mbali na hayo utawala wa Saudi Arabia na nchi kadhaa za Kiarabu za eneo mwaka 2021 zilitoa mashinikizo makubwa dhidi ya Lebanon na hivyo kuzidisha matatizo yake ya kiuchumi na kisiasa.
Lakini pamoja na hayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliamua kutuma mafuta yake katika nchi hiyo tena katika mazingira magumu ya kiusalama na vitisho vya Marekani, ili kujaribu kupunguza machungu ya watu wa nchi hiyo na ingali inaendeleza siasa hizo za kiutu na kidugu kwa nchi hiyo ya Kiarabu. Kuhusu hilo, Hossein Amirabdollahian, huku akisisitiza kudumishwa kwa siasa hizo za kupunguza machungu ya Walebanon hasa katika nyanja za msaada wa umeme na nishati amesema kuwa Iran iko tayari kukarabati mitambo ya kuzalisha umeme na kujenga mingine mipya katika nchi hiyo.
Suala jingine muhimu ni kwamba Tehran na Beirut zina mitazamo inayofanana kuhusiana na uchokozi wa siku zote wa utawala wa kigaidi wa Israel ambapo mbali na kulaani jinai za utawala huo dhidi ya Wapalestina, zinasisitiza kudumishwa mapambano dhidi ya utawala wa Tel Aviv. Kwa msingi huo na katika mazungumzo yake na waziri mwezake Amirabdollahian, Abdallah Bou Habib amesema kuwa mitazamo ya Iran na Lebanon kuhusu baraza jipya la mawaziri la Israel ni mimoja na kuongeza: Sisi tumelaani vikali hatua ya hivi karibuni ya waziri wa usalama wa ndani wa Israel ya kuingia katika Msikiti wa al-Aqsa na tunaitaka jamii ya kimataifa itekeleze majukumu yake ya kuuzuia utaweala wa Israel kuendelea kuuvunjia heshima Masjidul Aqsa.