Jeshi la Iraq laingia katikati mwa mji wa Fallujah, Daesh wakimbia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i9361-jeshi_la_iraq_laingia_katikati_mwa_mji_wa_fallujah_daesh_wakimbia
Ripoti za hivi karibuni zinasema kuwa jeshi la Iraq na wapiganaji wa kujitolea wamefanikiwa kuingia katikati mwa mji wa Fallujah uliokuwa ukidhibitiwa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh kwa miaka kadhaa sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 17, 2016 03:42 UTC
  • Jeshi la Iraq laingia katikati mwa mji wa Fallujah, Daesh wakimbia

Ripoti za hivi karibuni zinasema kuwa jeshi la Iraq na wapiganaji wa kujitolea wamefanikiwa kuingia katikati mwa mji wa Fallujah uliokuwa ukidhibitiwa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh kwa miaka kadhaa sasa.

Ripoti zinasema wapiganaji wa kundi hilo wamechanganyikiwa na kuanza kukimbia ovyo.

Ofisi ya operesheni ya kukomboa mji wa Fallujah imetangaza kuwa, wapiganaji wa kundi hilo la kigaidi wanatoroka mji huo kwa wingi na kwamba wanakimbilia katika maeneo ya al Halabisa na al bu-Alwan magharibi mwa mji huo.

Ofisi hiyo imetangaza kuwa operesheni iliyofanyika kwa mafanikio ya kuwaondoa raia wa kawaida katika mji wa Fallujah imesaidia sana katika kufanikisha ushindi wa jeshi la Iraq na makundi ya kujitolea dhidi ya magaidi hao.

Kwa sasa jeshi la Iraq linafanya jitihada za kukomboa na kusafisha majengo yote ya umma yaliyokuwa yakidhibitiwa na kundi la Daesh.

Jeshi la Iraq lilianza operesheni ya kukomboa mji wa Fallujah tarehe 23 Mei mwaka huu. Mji huo unahesabiwa kuwa miongoni mwa ngome kuu za kundi hilo la kigaidi.