Jun 20, 2016 05:24 UTC
  • 30,000 wafurushwa Fallujah Iraq katika muda wa siku 3 zilizopita

Baraza la Wakimbizi la Norway limesema kwa akali watu 30,000 wamelazimika kuyahama makazi yao katika mji wa Fallujah nchini Iraq katika muda wa siku 3 zilizopita kutokana na kushtadi mapigano katika mji huo wa kistratajia kati ya vikosi vya jeshi na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS).

Taarifa iliyotolewa na baraza hilo jana Jumapili imesema kuwa, zaidi ya watu 30,000 wamehama makazi yao na kukimbilia meneo salama nchini Iraq, kutokana na vikosi vya serikali kuimarisha operesheni zao katika mji huo ulioko yapata kilomita 69 magharibi mwa mji mkuu Baghdad.

Nasr Muflahi, Mkurugenzi wa Baraza la Wakimbizi la Norway nchini Iraq amesema kuwa, watu wengine 32,000 tayari walikuwa wameukimbia mji huo baada ya vikosi vya serikali kuanzisha operesheni kali dhidi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika mji huo mwezi mmoja uliopita. Ameitaka serikali kulishughulikia suala hilo la kibinadamu kabla mambo kuharibika zaidi.

Mapema Ijumaa, jeshi la Iraq na wapiganaji wa kujitolea walifanikiwa kuukomboa mji wa Fallujah kutoka mikononi mwa wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh. Jeshi la Iraq lilianza operesheni ya kukomboa mji wa Fallujah tarehe 23 Mei mwaka huu. Mji huo ulikuwa unahesabiwa kuwa miongoni mwa ngome kuu za kundi hilo la kigaidi.

Tags