Hamas: Jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel hazitapita bila jibu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i95804-hamas_jinai_za_utawala_wa_kizayuni_wa_israel_hazitapita_bila_jibu
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani mauaji yanayofanywa na askari wa utawala haramu wa Israel dhidi ya vijana wa Kipalestina katika Msikiti wa Al-Aqsa na kutangaza kuwa uhalifu huo hautapita bila kujibiwa.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 02, 2023 04:24 UTC
  • Hamas: Jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel hazitapita bila jibu

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani mauaji yanayofanywa na askari wa utawala haramu wa Israel dhidi ya vijana wa Kipalestina katika Msikiti wa Al-Aqsa na kutangaza kuwa uhalifu huo hautapita bila kujibiwa.

Ni baada ya askari wa Israel kumuua shahidi Mohammad al-Asibi, Mpalestina aliyekuwa na umri wa miaka 26 mkaazi wa kijiji cha Hora katika eneo la Negev linalokaliwa kwa mabavu. Kijana huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel karibu na Bab al-Salsala jana jioni alipojaribu kumhami mwanamke wa Kipalestina dhidi ya mashambulizi ya wanajeshi makatili wa Israel.

Taarifa iliyotolewa na harakati ya Hamas imeeleza kuwa, jinai za wavamizi wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina hazitapita bila jibu na kuongeza kuwa: Taifa letu litashikamana na ahadi yake kwa mashahidi na kuendeleza mapambano. 

Hapo awali harakati ya Jihad Islami ya Palestina ilikuwa tayari imetoa taarifa ikilaani kuuawa shahidi vijana wa Kipalestina mikononi mwa Wazayuni katika Msikiti wa Al-Aqsa na kusisitiza umuhimu wa kuendelezwa mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Palestina dhidi ya jinai hizo za kinyama.

Licha ya hujuma na vikwazo vikali vya utawala wa Kizayuni wa Israel, waumini zaidi ya laki mbili na nusu wanahudhuria Swala za Isha na Tarawehe katika Msikiti wa Al-Aqswa. Malaki ya Waislamu pia walishiriki katika Swala ya pili ya Ijumaa ya Mwezi wa Ramadhani katika Msikiti wa Al-Aqsa.