Idi ya muqawama; siku ya jinamizi kwa wavamizi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i98010-idi_ya_muqawama_siku_ya_jinamizi_kwa_wavamizi
Tarehe 25 Mei mwaka 2000, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulishindwa vibaya sana kwa kipigo kikali ulichopata kwa Muqawama wa Hizbullah ya Lebanon; na matokeo yake ukalazimika kurudi nyuma na kuondoka kimadhila kusini mwa nchi hiyo. Siku hiyo imekuwa maarufu nchini Lebanon kwa la jina la "Sikukuu ya Muqawama".
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 26, 2023 22:09 UTC
  • Idi ya muqawama; siku ya jinamizi kwa wavamizi

Tarehe 25 Mei mwaka 2000, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulishindwa vibaya sana kwa kipigo kikali ulichopata kwa Muqawama wa Hizbullah ya Lebanon; na matokeo yake ukalazimika kurudi nyuma na kuondoka kimadhila kusini mwa nchi hiyo. Siku hiyo imekuwa maarufu nchini Lebanon kwa la jina la "Sikukuu ya Muqawama".

Katika kuadhimisha siku hii, kila mwaka Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon huandaa hafla na sherehe maalumu katika siku hii ambayo kimsingi ni mwanzo wa kushindwa mtawalia jeshi la Israel na wakati huo huo ni mwanzo wa ushindi juu ya ushindi kwa harakati za muqawama katika eneo la Asia Magharibi.

Sherehe za mwaka huu za kusherehekea ushindi wa kihistoria wa Hizbullah ya Lebanon wa mwaka 2000 ziliambatana na luteka maalumu ya kijeshi ambayo sio tu kwamba, zilionyesha mandhari maalumu ya sherehe hizi, bali zimeibua daghadagha na kihoro kipya kwa utawala ghasibu wa Israel.

Jumapili ya tarehe 21 Mei, sambamba na kukaribia maadhimisho ya mwaka wa 23 wa kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon, Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon ilifanya mazoezi makubwa ya kijeshi kwa lengo la kuonyesha utayarifu wa muqawama wa kuilinda ardhi ya Lebanon.

Katika manuva ya kijeshi ya aina yake ambayo hayajawahi kushuhudiwa, ambayo yalifanywa mbele ya mamia ya waandishi wa habari, Muqawama wa Lebanon ulionyesha sehemu ndogo tu ya uwezo wake wa kiufundi na kijeshi huko kusini mwa nchi hiyo na kwenye mpaka wa pamoja na Palestina inayokaliwa kwa mabavu iliyopewa jina la Israel. Mazoezi hayo yalifanyika chini ya anuani ya "Sisi Tutapita ... Kwa hiyo tumo katika hali ya kupita"; kaulimbiu ambayo inafikisha jumbe nyingi na maalumu kwa Wazayuni maghasibu.

Wanamapambano wa Hizbullah ya Lebanon

Mazoezi hayo ya kijeshi ya Hizbullah yalikuwa tukio la kusisimua mno kwa maripota, waandishi habari na wapiga picha zaidi ya 650 kutoka Lebanon na nje ya nchi hiyo ambao walihudhuria na kujionea kwa macho yao kwenye uwanja wa manuva hayo, kufuatia mwaliko uliotolewa na kitengo cha habari cha harakati hiyo. Mazoezi hayo yamedhihirisha utayari wa Hizbullah wa kujitosa kwenye ulingo wa makabiliano yoyote yale ya kijeshi na adui.

Katika mazoezi hayo ya kijeshi ambayo wengi wameyatafsiri kama onyo maalumu kwa utawala haramu wa Kizayuni, Hizbullah ilionyesha sehemu ndogo tu ya uwezo wake wa kijeshi, kwa kutumia silaha za aina mbalimbali yakiwemo makombora ya kutungulia vifaru yaliyofungwa kwenye magari mepesi, mitambo ya kurushia maroketi ya masafa na ukubwa tofauti, magari ya kivita ya deraya, ndege zisizo na rubani za droni n.k.

Kwa kuzingatia kwamba, wiki chache zilizopita, serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani ilitangaza kuwa, haitazuia shambulio la Israel dhidi ya taasisi za nyuklia za Iran na tamko hilo ni kupatiwa idhini na baraka serikali ya Benjamin Netanyahu, hivyo, ujumbe na utendaji muhimu wa maonyesho haya ya kijeshi ya Hizbullah unaweza kutathminiwa kuwa ni kuonyesha nguvu mbele ya vitisho vya adui.

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon

Katika mazoezi hayo ya kijeshi, Muqawama wa Lebanon ulitekeleza pia operesheni ya mshabaha wa kuingia eneo la kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kulidhibiti eneo la Al-Khalil (Galilaya), hatua ambayo ni jinamizi kubwa zaidi kwa Wazayuni. Katika mazoezi hayo, wapiganaji waliovalia sare za madoadoa huku wakiwa wamefunika nyuso zao wa kikosi maalumu cha Ridhwan, ambacho kinazishughulisha mno na kuzikosesha raha duru za Israel, walikaa kwenye magari na kuonyesha ustadi na uwezo wao mkubwa wa kukabiliana na adui mzayuni mbele ya kamera za mamia ya waandishi wa habari wa ndani na nje ya Lebanon.

Miongoni mwa jumbe na salamu walizopokea Wazayuni kutokana na manuva ya Hizbullah kama walivyokiri wataalamu wa utawala huo, ni sisitizo hilo la kuwepo umoja wa kambi zote za muqawama kuanzia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hadi Lebanon na Palestina, Yemen, Syria, Iraq na makundi yote ya mapambano na Muqawama katika ukanda huu wa Asia Magharibi. Hii ina maana kwamba, vita vyovyote katika mustakabali vitajumuisha makundi yote ya muqawama yakiwa na utendaji ulio na umoja na mshikamano dhidi ya adui.