Imran Khan: Masaibu yangu yametokana na kuipa mgongo Marekani
Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan, Imran Khan ameituhumu Marekani kwa kula njama iliyopelekea kuangushwa kwa serikali yake iliyochaguliwa kidemokrasia.
Khan amesema hayo katika mahojiano na gazeti la Newsweek, ambapo mbali na kukosoa undumakuwili wa nchi za Magharibi, amesema misimamo yake ya kupinga na kupuuza sera za Marekani ndiyo iliyopelekea kuporomoka kwa serikali yake.
Mwanasiasa huyo wa chama cha upinzani cha PakistanTehreek-e-Insaf (PTI) amesema, "Wamarekani hawakufurahishwa na sera zangu huru za mambo ya nje na hatua yangu ya kuitembelea Russia, na kwa msingi huo wakapika majungu ya kisiasa ili kunisawiri kama adui wa Marekani."
Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan amesema ana ushahidi wa kimaandishi unaothibitisha kuwa Marekani kwa muda mrefu ilipanga njama za kumuondoa madarakani.
Khan amekosoa undumakuwili na unafiki wa Marekani wa kutokubali kukosolewa na kuongeza kuwa, "Kutokana na sababu fulani, iwapo haukubaliana na sera ya nje ya Washington, unaonekana kuwa adui wa Marekani."
Khan aliondolewa katika wadhifa wa uwaziri mkuu katika kura ya kutokuwa na imani naye aliyopigiwa na Bunge la nchi hiyo mwaka uliopita 2022, uamuzi ambao anasisitiza ulitokana na njama iliyoongozwa na Marekani na jeshi.
Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Pakistan amedai kuwa, kukamatwa kwake pamoja na viongozi wengine wa chama chake kulionyesha nguvu nyingi zinazotumiwa na jeshi la Pakistan na wakala wake wa shirika la intelijensia (ISI).