Marekani na kukana mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza
Zaidi ya mwezi mmoja umepita sasa tangu kuanza kwa vita vya Gaza na tangu kutekelezwa kwa operesheni ya "Kimbunga cha Al-Aqsa" huku utawala wa Kizayuni unaoendesha operesheni za ardhini katika Ukanda wa Gaza dhidi ya wapiganaji wa Hamas ukizidisha mashambulizi yake ya anga dhidi ya eneo hilo. Mashambulio hayo ya kinyama ya Israe; yameendelea kusababisha mauaji makubwa ya watu wanaodhulumiwa wa Ukanda wa Gaza.
Mashambulio hayo ya kinyama ya Israe; yameendelea kusababisha mauaji makubwa ya watu wanaodhulumiwa wa Ukanda wa Gaza.
Ingawa idadi ya mashahidi wa Palestina imezidi elfu 10 na waliojeruhiwa wamezidi 24,000, na sehemu kubwa ya mashahidi hao ni watoto na wanawake, lakkini Marekani ikiwa muungaji mkono mkuu na asiye na masharti wa Israel, imetoa madai ya kushangaza na kukanusha waziwazi kutokea mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kuhusiana na hilo John Kirby, msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa la Ikulu ya White House akiunga mkono jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina amedai kuwa, kinachoendelea Gaza si mauaji ya kimbari. Kirby amesema: Huwezi kuangalia matukio ya Gaza na kusema kwamba, matukio haya yanakidhi fasili na maana ya mauaji ya kimbari. Aliendelea kudai kwa kusema, neno "mauaji ya kimbari" ni "mbinu ya kutowajibika ya kuelezea matukio."

Afisa huyu wa Marekani anapaswa kuulizwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ambao kimsingi umefanya mauaji makubwa mno ya watu wa Ukanda wa Gaza ambayo hayajawahi kushuhudiwa kwa kisingizio cha kujilinda na inaungwa mkono kikamilifu na utawala wa Biden na Kongresi ya Marekani katika suala hili, ni jinai gani ambayo inapaswa kufanywa na utawala huo hata iwe ni kielelezo cha jinai za kivita na mauaji ya kimbari?
Pia, madai ya Kirby kuhusu kutotokea mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza yameibuliwa huku hata Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) umekiri kuuawa kwa umati Wapalestina. Msemaji wa Pentagon Patrick Ryder hatimaye alikiri baada ya mwezi mmoja tangu kuanza kwa mapigano kati ya makundi ya muqawama wa Palestina na Israel kwamba, maelfu ya raia wameuawa na kujeruhiwa katika Ukanda wa Gaza katika hatua ya Tel Aviv ya kulipiza kisasi dhidi ya operesheni ya kimbunga ya Al-Aqsa.
Patrick Ryder alikiri Jumatatu ya juzi kwamba: "Kuhusu yaliyowakumba raia huko Gaza, tunajua waliouawa ni maelfu."
Jeshi la Anga la Kizayuni hadi sasa limetumia tani 35,000 za mada za milipuko ambazo ni zaidi ya mara mbili ya uwezo wa bomu la atomiki la Hiroshima kulenga maeneo mbalimbali za Ukanda wa Gaza.
Ukubwa wa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina umepelekea hata baadhi ya viongozi waandamizi wa Ulaya kuonyesha hasira zao kwa jinai hizo.

Caroline Gennez, Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Ubelgiji ametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu jinai za kivita zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza. Akizungumza katika mahojiano ya televisheni Jumatatu usiku, Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Ubelgiji aligusia jinai na uhalifu unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Gaza na kusema: "Israel inapasa kuchunguzwa kwa kufanya jinai za kivita, na ushahidi uliopo unanyesha kuwa utawala huo umetenda uhalifu wa kivita."
Nukta muhimu ni kwamba, licha ya msimamo wa Rais wa sasa Marekani na utawala wake kuwa muungaji mkono asiye na masharti na wa pande zote kwa Israel na jaribio la kuwalaumu Wapalestina hususan Hamas kwa kuanzisha vita vya sasa vya Gaza, lakini hata wanasiasa wa Marekani, wanafahamu vyema utambulisho wa kivamizi wa utawala wa Kizayuni na ukandamizaji wa miongo kadhaa wa Wazayuni dhidi ya Wapalestina ambao umeendelea hadi sasa kwa kuua na kupora ardhi zao na hivyo wamejitokeza na kukosoa jambo hilo.
Kuhusiana na hilo, wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani katika risala yao wamekosoa namna serikali ya Marekani ilivyosimamia vita kati ya utawala wa Kizayuni na Hamas na kutangaza kuwa, utawala wa Biden unapaswa kuikosoa hadharani Israel.

Hii ni katika hali ambayo, misimamo isiyo ya haki na ya uungaji mkono ya serikali ya Biden kwa utawala wa Kizayuni imewafanya baadhi ya wanasiasa huru wa Marekani na hata wanasiasa wa chama kinachotawala cha Democrats kukosoa misimamo ya uungaji mkono ya serikali ya Biden kwa utawala wa Kizayuni. Rashida Tlaib, mjumbe wa chama cha Democratic katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, alisema Jumamosi: Joe Biden ameunga mkono "mauaji ya halaiki" dhidi ya Wapalestina katika vita vya Gaza, na Wamarekani hawatasahau suala hili katika uchaguzi wa mwakka ujao nchini Marekani.
Bernie Sanders, Seneta wa kujitegemea anayewakilisha jimbo la Vermont nchini Marekani amelaani "mauaji ya upofu ya watu wasio na hatia" huko Palestina na kusema kwamba, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni lazima yakomeshwe.
Licha ya misimamo hiyo ya ukosoaji, lakini serikali ya Biden na Bunge la Congress la Marekani zinaendelea kuuunga mkono utawala wa Kizayuni. Kuhusiana na suala hilo, serikali ya Biden inapanga kutuma huko Israel mabomu madogo lakini yenye umakini mkubwa na ambayo yana thamani ya dola milioni 320.