Nov 08, 2023 06:09 UTC
  • 40% ya wanaume Waislamu Ujerumani wanakabiliwa na ubaguzi

Utafiti mpya umefichua kuwa, asilimia 40 ya wanaume Waislamu nchini Ujerumani wanakabiliwa na vitendo vya ubaguzi katika maisha yao ya kila siku, huku hujuma na mashambulio ya kibaguzi dhidi ya Waislamu yakiripotiwa kukithiri katika nchi hiyo ya bara Ulaya.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa jana Jumanne mjini Berlin na Kituo cha Utafiti wa Utangamano na Uhamiaji cha Ujerumani  (Dezim), asilimia 41.2 ya wanaume wafuasi wa dini ya Kiislamu wanaandamwa na ubaguzi kila siku kwa misingi ya imani yao.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa: Thuluthi moja ya wanaume Waislamu (39%) wameripoti kushuhudia kesi za ubaguzi wa rangi mikononi mwa polisi, na asilimia 51 katika ofisi za umma na wanapozungumza na mamlaka za nchi hiyo.

Utafiti wa Dezim umefichua kuwa, asilimia 46 ya wanawake Waislamu nchini humo wanakabiliwa na aina moja au nyingine ya ubaguzi kila siku katika ofisi za umma na taasisi za serikali.  

Mkurugenzi wa Taasisi ya Dezim,  Frank Kalter ​anasema: Ubaguzi wa rangi ni sehemu ya maisha ya kila siku kwa Waislamu nchini Ujerumani, na ubaguzi huo unafanyika kwa njia tofauti ikiwemo katika utoaji wa huduma za afya.

Wanawake Waislamu nchini Ufaransa wanashuhudia visa vya ubaguzi na chuki dhidi yao

Ripoti hii imetolewa siku chache baada ya Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani kudai kwamba, Uislamu ni dini ya Ujerumani; huku kukiwa na ongezeko la ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu inayochochewa na propaganda za vikundi vya mrengo mkali wa kulia, na vyama ambavyo vimetumia vibaya mzozo wa wakimbizi na kujaribu kuzua hofu dhidi ya wahamiaji.

Jumla ya matukio 898 ya chuki dhidi ya Uislamu yalirekodiwa nchini Ujerumani mwaka wa 2022, huku idadi ya kesi ambazo hazijaripotiwa ikiwa kubwa. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mwezi Juni na shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu mjini Berlin, Alliance Against Islamophobia and Muslim Hostility. 

Miongoni mwa kesi zilizorekodiwa ni pamoja na mashambulizi 500 ya maneno, ikiwa ni pamoja na kauli za uchochezi, matusi, vitisho na kulazimishwa. 

Tags