Watumishi wa umma Uholanzi waandamana wakitaka kusitishwa vita Gaza
Makumi ya wafanyakazi wa umma nchini Uholanzi jana Ijumaa waliwashangaza wengi kwa kuingia mabarabarani kushiriki maandamano ya kutaka kutekelezwa usitishaji vita wa kudumu katika Ukanda wa Gaza.
Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, watumishi hao wa umma walikusanyika nje ya Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo mjini Hague kushiriki maandamano hayo nadra ya kulaani jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
Waandamanaji hao wamekosoa kimya cha serikali yao mkabala wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Gaza. Washiriki wa maandamano hayo waliokuwa wamebeba bendera za Palestina wamesema hatua ya serikali ya Hague kufumbia macho jinai zinazofanyika Gaza inatia wasiwasi.
Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya NOS ya Uholanzi, ni nadra kwa maandamano kushuhudiwa katika nchi hiyo ya Ulaya.
Mwezi Oktoba mwaka huu, watumishi wa umma nchini Uholanzi waliiandikia barua serikali ya nchi hiyo, wakiitaka iilazimishe Israel isitishe mashambulizi yake dhidi ya watu wa Gaza.

Jana Ijumaa pia, wananchi wa Yemen, kwa mara nyingine tena walifanya maandamano makubwa ya kulaani jinai na mashambulizi ya kinyama ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
Kwa mujibu wa Press TV, maandamano hayo yalifanyika katika miji mbalimbali ya Yemen, ukiwemo mji mkuu Sana'a, ambapo waandamanaji pia walionyesha mshikamano wao na taifa la Palestina.
Wananchi wa Yemen walioshiriki katika maandamano hayo walikuwa wamebeba bendera za Yemen na Palestina, na mabango yenye jumbe za kulaani jinai za Israel na washirikia wake huko Gaza.