Feb 06, 2024 11:00 UTC
  • Russia, China: US inahatarisha usalama wa Asia Magharibi

Russia na China zimelaani vikali mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya Iraq na Syria na kusisitiza kuwa, Washington ni tishio kwa usalama wa eneo zima la Asia Magharibi.

Vassily Nebenzia, Balozi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, "Kwa mara nyingine tena, mashambulio hayo ya mabomu yamedhihirisha dhati ya sera za kiuhasama za Marekani Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) na mapuuza ya Washington kwa sheria za kimataifa."

Mwanadipomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia amebainisha kuwa: Marekani 'inamimina mafuta' kwenye moto, kwa kufanya hujuma za anga zenye hatari ya moja kwa moja kwa amani na usalama wa dunia, mbali na kudunisha jukumu kuu la Umoja wa Mataifa." 

Wakati huo huo, Zhang Jun, Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa amekosoa vikali pia mashambulizi hayo yanayoendelea kufanywa na Marekani na Uingereza katika nchi za Iran na Syria.

Vassily Nebenzia, Balozi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa

Amesisitiza kuwa, "Hakuna shaka hatua hizi za kijeshi za Marekani zinachochea mgogoro mpya katika eneo, sambamba na kushadidisha migogoro iliyokuwepo."

Naye Balozi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani jana Jumatatu alipohutubia kikao hicho cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu tishio la amani na usalama wa kimataifa alisema, mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani dhidi ya Iraq na Syria ni kinyume cha sheria na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Kabla ya hapo pia, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell alieleza wasiwasi wake kuhusu athari mbaya za mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya Syria na Iraq kwa hali inayogubikwa na wasiwasi ya eneo la Asia Magharibi, na kuonya kwamba hatua hizo zinaweza kuzidisha mivutano na kupanua wigo wa migogoro.

Tags