Mar 13, 2024 02:10 UTC
  • Kuendelea himaya ya Marekani kwa Israel; kuongezeka mashahidi wa Kipalestina katika anga ya uhaba wa chakula na dawa

Kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni katika kivuli cha uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo na kufungwa njia za kufikisha misaada na kuingia chakula na dawa katika Ukanda wa Gaza kumesababisha kuongezeka la idadi ya mashahidi wa Palestina.

Si hayo tu, bali hali hiyo imelifanya tatizo la uhaba wa chakula na dawa kuzidi kuchukua wigo mpana zaidi siku baada ya siku. Kuhusiana na hilo, Shirika la Haki za Binadamu la Ulaya-Mediterania limetangaza kuwa, wazee kaskazini mwa Gaza wanakufa mmoja baada ya mwingine kwa milipuko ya mabomu au kwa sababu ya njaa na ukosefu wa huduma za matibabu.

Idadi ya mashahidi huko Gaza imefikia zaidi ya watu elfu 31, ambapo 92% kati yao wakiwa ni raia. Pia, maelfu ya watu wamekufa kutokana na njaa, utapiamlo na ukosefu wa huduma za matibabu, ambapo majina yao hayajasajiliwa katika hospitali. Hali katika Gaza ni mbaya na kwa hakika utawala wa Kizayuni unaendelea na jinai zake dhidi ya Wapalestina kwa idhini na uungaji mkono wa Marekani, na licha ya matakwa ya walimwengu ya kutaka kusimamisha mashambulizi ya Israel, lakini Washington imeendelea kuiunga mkono Tel Aviv na hivyo kudumisha unafiki na undumakuwili wake.

Katika matamshi yanayokinzana na kugongana, Rais wa Marekani amelitaja shambulio la Israel dhidi ya Rafah, kusini mwa Gaza, kuwa ni "mstari mwekundu" ambao haupaswi kuvukwa, lakini wakati huo huo amesema kwamba, hana mstari mwekundu katika kuuunga mkono utawala wa Kizayuni na kwamba ni muhimu sana kuulinda utawala huo. Biden amesisitiza kuwa,  kuhusu mstari mwekundu wa Washington kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema kuwa kuilinda  Israel ni jambo muhimu na hakuna mstari mwekundu wa kuacha kutuma silaha kwa utawala huo.

Zaidi ya Wapalestina 30,000 wameuawa shahidi tangu Israel ianzishe mashambulio ya kinyama huko Gaza

 

Kimsingi ni kuwa, tangu kuanza kwa vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza, Marekani imekuwa muungaji mkono mkuu wa utawala ghasibu wa Israel na imeipatia Tel Aviv msaada mkubwa wa kisiasa, kiuchumi, kijeshi na silaha.

Uungaji mkono wa Washington umepelekea juhudi za kusimamisha mapigano Gaza kukwama na kufeli. Washington imezuia mara kwa mara kupitishwa kwa maazimio ya Umoja wa Mataifa ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano pamoja na utatuzi wa kidiplomasia wa kukomesha mauaji ya Wapalestina yanayofanywa na utawala haramu wa Israel.

Himaya na uungaji mkono huo umeifanya Israel ifanye waziwazi mauaji ya halaiki dhidi ya wakaazi wa Gaza na kutoheshimu hata haki za kimsingi kabisa za watu wa eneo hilo. Njaa na kufunga vivuko vya kuingia chakula pamoja na kukatwa misaada kutoka kwa mashirika ya kimataifa kama vile UNRWA pia ni hatua ambazo ziko katika mkondo huo.

Kuchukua wigo mpana zaidi jinai za Israel kumesababisha mashinikizo ya mitazamo ya umma duniani kuongezeka dhidi ya viongozi wa nchi za Ulaya na Marekani, kiasi kwamba viongozi wengi wa nchi za Ulaya licha ya kumuunga mkono Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu wa Kizayuni, lakini wanakosoa sera zake na kutaka kukomeshwa mauaji haya ya kimbari na jinai hizi dhidi ya Wapalestina.

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuhusiana na suala hili: "Ikiwa unaamini kwamba watu wengi wanauawa huko Gaza, labda unapaswa kupeleka silaha kidogo ili kuzuia vifo vya idadi kubwa ya watu."

Pamoja na hayo, Marekani inaendeleza uungaji  mkono wake wa Israel. Ingawa viongozi wa Washington wanajaribu kuweka mstari mwekundu kwa utawala wa Kizayuni mbele ya maoni ya umma, lakini kivitendo wanaipatia Israel silaha zinazohitajika na kufanya mambo kwa kuzingatia maslahi ya Tel Aviv. Utendaji huu wa kinafiki na kindumakuwili umeifanya Marekani ikabiliwe na ukosoaji hata kutoka kwa washirika wake.

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya

 

Katika uwanja huu, Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya sanjari na kukosoa vikali sera za Marekani amesema: "Ikiwa jamii ya kimataifa inaamini kuwa, haya ni mauaji na kuna watu wengi wanauawa, labda tunapaswa tufikirie juu ya suala la kudhamini silaha na zana za kivita.

Ndani ya Marekani, raia wengi, mashirika ya kiraia na maafisa wa kisiasa wamekuwa wakipaza sauti kuitaka serikali ya Biden isitishe uungaji mkono wake kwa Israel. Katika muktadha huo, Bernie Sanders, seneta wa jimbo la Vermont anasema: Washington ni mshirika katika maafa ya kibinadamu huko Gaza kutokana na kutoa msaada wa kifedha kwa Israel."

Vita vya Israel dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza vinaendelea, na inaonekana kuwa Israel, ikiwa na uhakika wa kuungwa mkono na Marekani, inaendelea kuua, na mamlaka za Marekani zinajaribu tu kupunguza mashinikizo ya umma dhidi yao kwa misimamo yao kindumakuwili.

Tags