Apr 06, 2024 09:21 UTC
  • Siku ya Quds ya aina yake; Kimbunga cha al Ahrar dhidi ya utawala dhalimu wa Kizayuni

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu yamekuwa tofauti sana ikilinganishwa na miaka iliyopita; ambapo wananchi katika nchi mbalimbali duniani wameshiriki kwa wingi katika maadhimisho hayo ikiwemo hapa nchini Iran.

Siku ya Kimataifa ya Quds imetokana na ubunifu wa Iran wenye sura ya kimataifa na kuzishirikisha nchi mbalimbali. Imam Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran miezi sita tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds kupitia ubunifu wake huo wa kihistoria. Ubunifu huo ni moja ya sababu za kusalia hai kadhia ya Palestina. Hata hivyo Siku ya Kimataifa  ya Quds imesaidia vipi kubaki hai suala la Palestina?  

Siku ya Kimataifa ya Quds si siku ya maadhimisho ya serikali bali ni siku ya mataifa na wapigania uhuru na ukombozi duniani kote. Siku hii si ya nchi fulani tu bali ni ya wapigania ukombozi wote duniani wakiwemo Waislamu na wasio Waislamu. Lengo kuu la maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds ni kuwafahamisha walimwengu kuhusu suala la Palestina, na ili kwa upande mmoja watambue jinai zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina na kwa upande wa pili, lengo ni kuwashawishi watu duniani kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina. Sayyid Abdulmalik al Houthi kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen alisema katika kukaribia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu kwamba:" Siku ya Kimataifa ya Quds ni hafla yenye lengo la kuongeza mwamko wa walimwengu na kuhuisha hisia ya uwajibikaji mkabala wa kadhia ya Palestina." 

Sayyid Abdul Malik al Houthi 

Matokeo ya mwamko huu yamedhihirika katika maandamano ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Quds. Jana Ijumaa wananchi katika nchi mbalimbali duniani waliadhimisha siku hii ya kukumbukwa. Wakati huo huo wananchi katika mikoa yote ya Iran walishiriki kwa wingi kwa kufanya maandamano makubwa jana katika maadhimisho ya Siku ya Quds. Wanawake na wanaume, wazee, vijana na watoto, Waislamu wa Shia na Suni na raia wa matabaka mbalimbali jana walishiriki kwa hamasa kubwa na kutangaza mshikamano wao na wananchi madhulumu wa Palestina.  

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds nchini Iran

Mbali na hapa nchini, wananchi katika maeneo na nchi mbalimbali duniani jana walishiriki kwa wingi katika maadhimisho ya Siku ya kimataifa ya Quds. Hii ni katika hali ambayo wananchi wa Yemen walifanya maandamano makubwa ya hamasa; ambapo mamilioni ya watu walishiriki katika maadhimisho hayo kwa ajili ya kuwaunga mkono na kuonyesha mshikamano na wananchi madhulumu wa Ukanda wa Gaza. Wananchi wa Jordan pia ambao juzi Alhamisi walifanya maandamano ya kuiunga mkono Palestina na kutaka kufutwa makubaliano ya amani kati ya nchi hiyo na utawala wa Kizayunim jana Ijumaa pia walishiriki kwa wingi katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds. Maandamano hayo hayakufanyika katika nchi za Kiislamu pekee. Wananchi katika nchi zisizo za Kiislamu pia ikiwemo Uingereza pia waliandamana jana kuiunga mkono Palestina na kuulani utawala wa Kizayuni.  

Nukta muhimu hapa ni kuwa maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds katika miaka iliyopita pia yamekuwa yakifanyika katika nchi mbalimbali hata hivyo mauaji ya kimbari ya miezi 6 ya karibuni yanayotekelezwa na utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza yametoa msukumo na kupelekea mwaka huu maandamano hayo kufanyika katika nchi nyingi zaidi na kwa ushiriki mkubwa wa wananchi ikilinganishwa na miaka iliyopita. Mahudhurio haya makubwa yanadhihirisha hasira na kuchukizwa walimwengu na jinai zinazofanywa na utawala dhalimu wa Kizayuni dhid ya watu wasio na hatia. Nasser Kanani Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aliashiria jana kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds jinai za miaka sabini na ushei za utawala haramu wa Kizayuni kwa himaya na uungaji mkono wa pande zote wa Marekani na Uingereza na kuandika: "Kile kilichotokea katika miezi 6 ya karibuni huko Ukanda wa Gaza uliotapakaa damu ni kufichuliwa wasifu mpya na wa kuchukiza wa kina cha ukatili na udhalimu wa utawala bandia wa Kizayuni mbele ya macho ya walimwengu."

Nasser Kanani 

Nukta ya mwisho ni kuwa; tunaweza kuyataja maandamano ya jana ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds katika nchi mbalimbali duniani kwa maana halisi ya Kimbunga cha al Ahrar au kimbunga cha wapigania ukombozi dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni  unaotekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.

Tags