Apr 24, 2024 02:44 UTC
  • Kamishna wa UN: Picha ya mtoto anayetolewa kwenye fuko la mama yake anayekata roho Ghaza ni zaidi ya tukio la vita

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amekemea vikali mashambulio ya kinyama na ya mfululizo yaliyofanywa hivi karibuni na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda Gaza na kuua zaidi wanawake na watoto.

Volker Turk ametoa kemeo hilo baada ya watoto wasiopungua tisa kati ya Wapalestina 16 kuuawa shahidi siku ya Jumapili katika shambulio la makombora ya ndege za kivita za la jeshi la Israel lililolenga makusudi nyumba kadhaa mashariki mwa Rafah kusini mwa Ukanda wa Ghaza.
 
Taarifa ya Turk iliyosomwa na msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN (OHCHR) Ravina Shamdasani mjini Geneva imesema: "picha za hivi punde za mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati wake aliyechukuliwa kutoka tumboni mwa mama yake anayekufa, za nyumba mbili zilizo karibu ambapo watoto 15 na wanawake watano waliuawa-ni zaidi ya tukio la vita".
 
Katika taarifa yake hiyo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza tena kwamba operesheni ya kuivamia kijeshi Rafah itasababisha uvunjifu zaidi wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, na vile vile ina hatari ya kusababisha vifo zaidi, majeruhi na uhamishaji mkubwa wa watu kwenye makazi yao au hata kufanyika uhalifu mkubwa zaidi wa kikatili, ambao watakaohusika nao watapasa kuwajibishwa.
Volker Turk

Aidha amesema "ameshtushwa" na uharibifu uliofanywa kwenye Hospitali ya Nasser na Hospitali ya Al Shifa na taarifa ya kugunduliwa makaburi ya halaiki karibu na maeneo haya na kutaka uchunguzi "huru, madhubuti na wa uwazi" ufanyike juu ya vifo hivyo.

 
Mili ipatayo 283 imefukuliwa hadi sasa kutoka kwenye kaburi la umati katika eneo la Jengo la Hospitali ya Nasser baada ya jeshi katili la utawala haramu wa Israel kuondoka katika mji huo Aprili 7 kufuatia mashambulizi ya ardhini ya miezi minne.
 
Kuhusu "ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu" unaoendelea kufanywa na Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, Turk amesema, licha ya kulaaniwa kimataifa mashambulizi makubwa ya walowezi wa Kizayuni ya kuanzia Aprili 12 hadi14 ambayo yaliwezeshwa na Vikosi vya Usalama vya Israeli (ISF), hujuma za walowezi hao dhidi ya raia wa Palestina wa eneo hilo zimeendelea kufanywa kwa usaidizi, ulinzi, na ushiriki wa ISF.../

 

Tags