May 27, 2024 02:19 UTC
  • Uamuzi wa Mahakama ya Hague kuhusu Rafah: Kushindwa kwingine kwa utawala wa Kizayuni

Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliyo na makao makuu yake mjini The Hague, Uholanzi , ambacho ni chombo cha juu zaidi cha mahakama cha Umoja wa Mataifa, iliamua Ijumaa, Mei 24, kwamba Israel lazima isimamishe "mara moja" mashambulizi yake ya kijeshi huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Mahakama hiyo iliamuru kwa kura 13 za ndio na kura 2 za kupinga, kusitishwa mara moja operesheni za kijeshi za utawala wa Kizayuni huko Rafah na kufunguliwa tena kivuko cha Rafah kwa ajili ya kuingizwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza. Kutokana na kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Gaza, Afrika Kusini wiki iliyopita iliitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kuiamuru Israel isitishe mara moja hujuma dhidi ya Rafah ikiwa ni hatua ya dharura na kusisitiza kuwa, hatua za Israel katika eneo la kusini mwa Gaza ni "mauaji ya halaiki" ambayo yanatishia maisha ya watu wa Palestina. Awali, Afrika Kusini ilikuwa imeituhumu Israel kwa kukiuka mkataba wa Umoja wa Mataifa wa "Mauaji ya Halaiki."

Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilisema kwamba uamuzi wake huo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa maisha ya watu wa Palestina yanalindwa. Jaji Nawaf Salam, mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, alisema kwamba Afrika Kusini iliiomba mahakama hiyo kuchukua hatua za ziada kutokana na hujuma kali ya operesheni za kijeshi za utawala ghasibu wa Israel huko Rafah. Kwa kauli yake na kwa mujibu wa Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari, operesheni yoyote ya Israel huko Rafah inaweza kusababisha uharibifu wa kiwango fulani au mkubwa katika mji huo, hivyo lazima Israel isimamishe mara moja mashambulizi yake ya kijeshi huko Rafah.

Hata kama chombo hiki cha mahakama cha kimataifa kinaweza kutoa maamuzi ya kisheria ya kutatua mizozo kati ya nchi, lakini hakina uwezo wa kuyatekeleza kivitendo. Pamoja na hayo, uamuzi wake dhidi ya utawala wa Kizayuni umeongeza mashinikizo ya kidiplomasia dhidi ya utawala huo ghasibu. Jambo la kuzingatiwa ni kuwa mara tu baada ya kutolewa uamuzi huo, utawala haramu wa Israel ulishambulia moja ya kambi za wakimbizi huko Rafah ili kuonyesha kuwa uamuzi wa mahakama hiyo hauna maana yoyote kwake.

Mahakama ya Kimataifa ya Haki yenye makao makuu yake The Hague.

Vitendo vya kijinai vya Israel katika vita vya Gaza hususan mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa ukanda huo viliifanya Afrika Kusini ikiwa miongoni mwa nchi zinazokosoa vikali jinai za utawala wa Kizayuni kuushtaki utawala huo katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ mwezi Disemba 2023 kwa kukiuka "Mkataba wa Mauaji ya Kimbari," hatua ambayo imeungwa mkono na makumi ya nchi nyingine kote ulimwenguni.

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pia imesisitiza uungaji mkono wake kamili kwa mashtaka yaliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa kufanya mauaji ya halaiki na kukiuka Mkataba wa Kupiga Marufuku Mauaji ya Umati wa 1948. Pia wataalamu na wahadhiri wa masuala ya sheria za kimataifa 200 wametangaza kuiunga mkono Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Hivi sasa, hukumu iliyotolewa karibuni na mahakama ya ICJ ya kusimamisha operesheni za kijeshi za utawala wa Kizayuni huko Rafah imepokelewa vizuri na nchi pamoja na taasisi za kieneo na kimataifa.

Harakati ya Hamas pia imekaribisha hukumu hiyo na kusema inatazamia kuwa mahakama hiyo itatoa amri ya kusimamisha vita katika ukanda mzima wa Gaza na sio tu Rafah na kuitaka iushinikize utawala wa Kizayuni ili uitekeleze mara moja.

Suala muhimu ni kuhusu msimamo wa Umoja wa Mataifa kuhusu uamuzi huo mpya wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki. Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, alisisitiza Ijumaa kwamba hukumu ya mahakama ya ICJ kwa Israel ya kusitisha operesheni za kijeshi huko Rafah ni "ya lazima" na kuwa pande zote zinapasa kuitekeleza bila kupoteza wakati.

Mashtaka ya ICJ dhidi ya Israel kuhusu Gaza

Ni wazi kwamba Marekani itapinga uamuzi huo kupitia kura yake ya turufu katika Baraza la Usalama kama ambavyo imekuwa ikifanya kuhusiana na rasimu ya azimio lolote linaloikosoa Israel.

Bila shaka, kwa kutilia maanani msimamo wa Umoja wa Ulaya, tayari ni wazi kwamba kuna tofauti ya maoni kati ya Brussels na Washington kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuhusu Rafah. Janes Lonarcic, Kamishna wa Kudhibiti Migogoro wa Umoja wa Ulaya amesisitiza juu ya utekelezwaji wa hukumu ya mahakama hiyo kuhusu kusitishwa operesheni za kijeshi huko Rafah na kusema: "Hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa Israel kwa ajili ya kusimamisha vita ni lazima itekelezwe, hivyo pande husika zinapaswa kuiheshimu." Naye Josep Burrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, pia amezungumzia hukumu hiyo na kusema kwamba Umoja wa Ulaya lazima uchague moja kati ya mawili, ima kuunga mkono taasisi za kimataifa au kuiunga mkono Israel.

Nukta muhimu ni kwamba licha ya vitisho na upinzani wa Marekani ikiwa ni mshirika wa kistratijia wa Israel dhidi ya taasisi za mahakama za kimataifa na hata kutishia kuwawekea vikwazo wafanyakazi wa tasisi hizo endapo zitatoa maamuzi yaliyo dhidi ya utawala wa Kizayuni, lakini hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na taasisi hizo zikiwemo mahakama za ICC na ICJ dhidi ya Israel zinathibitisha wazi kuwa Washington itakabiliwa na matatizo makubwa kimataifa katika kutekeleza vitisho hivyo, na hivyo kuendelea kutengwa katika eneo na kimataifa.

Tags