Colombia kusimamisha usafirishaji wa makaa ya mawe kwa utawala wa Kizayuni
Wizara ya Biashara ya Colombia imetangaza kuwa, katika kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na kulaani jinai za utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza, inasimamisha usafirishaji wa makaa ya mawe kwa utawala wa Kizayuni.
Colombia ililitambua taifa huru la Palestina tarehe 9 Agosti 2018, na katika muendelezo wa kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina, hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Nje ya Colombia ilitangaza katika taarifa kwamba nchi hiyo inakusudia kufungua tena ubalozi wake katika mji wa Ramallah huko Palestina ili kuongeza kiwango cha uhusiano wa pande mbili kati yake na Mamlaka ya Ndani ya Palestina.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Wanachuo wa Iran (ISNA), Rais wa Colombia, Gustavo Petro, naye pia ametangaza kuwa nchi hiyo itaacha kusafirisha makaa ya mawe inayopeleka kwa utawala wa Kizayuni hadi vitakapomalizika vita vya Ukanda wa Gaza.
Mwishoni mwa mwezi wa Februari mwaka jana, Colombia ilisimamisha ununuzi wake wote wa silaha kutoka kwa utawala wa Kizayuni na kutoa wito wa kususiwa kimataifa utawala huo katili unaofanya mauaji ya kimbari huko Ukanda wa Gaza na kuua watoto, wazee na wanawake wasio na hatia.
Katika jinai zake za hivi punde, utawala huo katili wa Kizayuni umeshambulia kwa makombora na mabomu kambi ya Nuseirat, katikati mwa Ukanda wa Gaza siku ya Jumamosi na kuua watu wasiopungua 210 na kujeruhi wengine 400.
Mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza ambayo yanaendelea kwa mwezi wa nane sasa hayajauletea faida yoyote utawala wa Kizayuni zaidi ya kushamirisha na kushadidisha chuki tu dhidi yake ulimwenguni kote.