Hollande: Mapambano dhidi ya ugadi yatachukua muda
Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema katika mkutano na vyombo vya habari katika mji wa Nice kuwa mapambano dhidi ya ugaidi yatachukua muda, kwa sababu adui angali anaendeleza mashambulizi yake.
Rais wa Ufaransa amesema kuwa, nchi yake itakuwa makini zaidi katika mapambano dhidi ya ugaidi. Amesema kuwa watu karibu 50 ambao walijeruhiwa jana katika shambulio la kigaidi la Nice wako mahututi. Rais Hollande ameongeza kuwa, watu walioshuhudia shambulio hilo la kigaidi hawatasahau tukio hilo la kutisha na la kinyama katika umri wao wote.
Rais wa Ufaransa ameashiria watu walioaga dunia na waliojeruhiwa katika tukio hilo na kueleza kuwa: Watoto wengi na raia wa nchi za nje ni miongoni mwa wahanga wa shambulio la jana usiku. Rais Francois Hollande amewashukuru askari usalama wa nchi hiyo kwa kutekeleza vyema majukumu yao.
Watu 84 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililofanywa jana usiku na mtu aliyeendesha lori na kuukanyaga umati mkubwa wa watu waliokuwa katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Bastille katika mji wa Nice kaskazini mwa Ufaransa.
Baadhi ya duru za habari zimearifu kuwa mtu aliyefanya shambulizi hilo ametambuliwa kwa jina la Mohamed Lahouaiej Bouhlel aliyekuwa na umri wa miaka 31 na kwamba alikuwa akiishi katika mji wa Nice.