Tovuti ya Uingereza: Utawala wa Marekani ni kipofu kiasi kwamba unamhami mtu kama Netanyahu
"Kuporomoka kwa dola kunakuwa jambo lisiloepukika mara tu watawala wake wanapopoteza kabisa hisia za jinsi walivyokuwa wapuuzi na wa kutisha", hivi ndivyo ilivyoandika tovuti ya Uingereza ya Middle East Eye ikizungumzia fedheha kubwa ya Congress ya Marekani ya kumkaribisha na kumpigia makofi nduli na Adolf Hitler wa zama hizi, Benjamin Netanyahu, anayeendelea kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza huko Palestina.
Tovuti hiyo imeandika kuwa, hivi sasa hakuna nchi hata moja duniani isipokuwa Marekani, ambayo idadi kubwa ya wawakilishi wake bungeni na katika Seneti wanampigia makofi kwa shangwe Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wakati jeshi lake linaendelea kufanya mauaji katika Ukanda wa Gaza.
Ripoti ya ya tovuti ya British Middle East Eye inashangaa kwamba ni vipi Netanyahu - ambaye katika kipindi cha miezi kumi iliyopita amesimamia mauaji ya Wapalestina wapatao 40,000, karibu nusu yao wakiwa wanawake na watoto - amekaribishwa kama shujaa katika Congress ya Marekani!
Tovuti ya British Middle East Eye imeongeza kuwa, Netanyahu ndiye aliyeharibu makazi ya Wapalestina wapatao milioni 2.3, na huenda ikachukua miaka 80 kuyajenga upya kwa gharama ya si chini ya dola bilioni 50. Yeye ndiye aliyeharibu hospitali na vyuo vikuu vyote vya Gaza na kuzishambulia kwa mabomu shule zake zote, na ni yeye ambaye Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu anataka akamatwe kwa tuhuma za kufanya uhalifu dhidi ya binadamu.
Middle East Eye imeongeza kuwa: Netanyahu aliyekaribishwa kama shujaa katika Congress ya Marekani, ndiye ambaye Mahakama ya Kimataifa ya Haki imesema serikali yake imekuwa ikifanya kazi ya kuimarisha utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid), na kusimamia kilichoelezwa na mahakama hiyo kuwa ni "mauaji ya kimbari," na bado hakupingwa isipokuwa na mtu mmoja tu katika ukumbi wa Congress.
Itakumbukwa kuwa, mwakilishi wa chama cha Democratic katika Congress ya Marekani, Rashida Tlaib alipinga hotuba iliyotolewa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika Congress, Jumatano iliyopita, na kutaka awajibishwe kwa mauaji ya kimbari yanayofanyika Ukanda wa Gaza.
Tlaib ambaye alivalia keffiyeh na bendera ya Palestina, wakati wa hotuba ya Netanyahu, aliinua juu bango jeusi lenye maneno "mhalifu wa kivita" katika upande mmoja, na "mtenda jinai ya mauaji ya kimbari" katika upande mwingine.
Middle East Eye imesisitiza katika ripoti yake kwamba: Zaidi ya hayo, kupokewa Netanyahu katika Congress ya Marekani ulikuwa ukumbusho kwamba vita vya sasa huko Gaza sio "vita" kati ya Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), au vita vya ustaarabu kati ya Israel, ulimwengu wa Kiyahudi-Kikristo na ulimwengu wa Kiislamu, kama Netanyahu anavyotaka kuwaaminisha walimwengu, bali ni vita vya ubeberu wa Marekani, na sehemu ya kampeni yake ya kijeshi kwa ajili ya "kuidhibiti wa dunia".