Borrell: Mauaji ya umati ya Israel Ukanda wa Gaza hayawezi kutetewa
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amelaani shambulio la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wa Palestina waliokuwa katika Swala ya Alfajiri katika shule ya al-Tabi’in katika mji wa Gaza.
Jeshi la utawala wa Israel unaotekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza, jana Jumamosi liliwashambulia raia wa Palestina waliokuwa katika ibada ya Swala ya Alfajiri katika shule ya al-Tabi'in katika kitongoji cha al Daraj mashariki mwa mji wa Gaza. Wapalestina zaidi ya 100 waliuawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa katika hujuma hiyo ya kinyama ya Israel.
Raia wa Palestina karibu 200 walikuwa katika Swala ya Alfajiri jana asubuhi waliposhambuliwa na ndege za kivita za jeshi la Israel.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Josep Borrell Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya (EU) ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba amepatwa na mshtuko kwa kuangalia picha za shambulio la Israel katika shule ya al Tabi'in katika mji wa Gaza ambapo ripoti zinasema kuwa makumi ya Wapalestina wameuawa shahidi katika hujuma hiyo ya kikatili.
Borell ameeleza wasiwasi wake kuhusu idadi ya waliouliwa shahidi katika hujuma ya kikatili dhidi ya shule ya al Tabi'iin huko Gaza na kusema wiki iliyopita jeshi la Israel ilizishambulia shule zisizopungua 10 na kwamba mashambulizi yote hayo hayawezi kuhalalishwa kwa hali yoyote ile.