Ufaransa yamuonya Trump kuhusu eneo la Greenland la Denmark
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, jana Jumatano alimtahaharisha Donald Trump kuhusu hatua yake ya kutishia "mipaka huru" ya Umoja wa Ulaya baada ya rais huyo mteule wa Marekani kukataa kutupilia mbali hatua za kijeshi za kutaka kuidhibiti Greenland, eneo linalojitawala la mwanachama wa Umoja wa Ulaya, Denmark.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesema kuwa Umoja wa Ulaya hautaruhusu mataifa mengine kushambulia mipaka huru ya wanachama wake.
Jean-Noel Barrot alisema haya jana akijibu maoni ya rais mteule wa Marekani, Donald Trump, kuhusu kulidhibiti eneo la Greenland huko Denmark. Greenland ni eneo linalojitawala la ufalme wa Denmark.
Jumatatu iliyopita Trump alipinga kuachana na hatua za kijeshi au za kiuchumi kama sehemu ya nia yake ya kutaka Marekani ilidhibiti eneo la Greenland, pamoja na Mfereji wa Panama.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesema kuwa haamini kwamba Marekani ingevamia kisiwa kikubwa cha Arctic ambacho kimekuwa sehemu ya Denmark kwa zaidi ya miaka 600 sasa.
"Ni wazi kuwa Umoja wa Ulaya hauwezi kuyaruhusu mataifa mengine ya dunia kushambulia mipaka yake huru; Sisi ni bara lenye nguvu," amesema Jean-Noel Barrot.
Hatua hizi za Trump zimeweka wazi ajenda zake za kujitanua katika maeneo mbalimbali duniani, wiki mbili kabla ya kuapishwa na kuwa Rais mpya wa Marekani tarehe 20 mwezi huu wa Januari.