Brazil yaishutumu US baada ya wahajiri waliofukuzwa kuwasili wakiwa wamefungwa pingu
Serikali ya Brazil imeeleza kughadhabishwa kwake baada ya makumi ya wahamiaji waliofukuzwa kutoka Marekani kuwasili kwa ndege wakiwa wamefungwa pingu, na kusema kuwa ni "kupuuzwa waziwazi" kwa haki zao.
Wizara ya Mambo ya Nje imesema katika taarifa kuwa, itaitaka Washington itoe maelezo rasmi kuhusu "vitendo hivyo vya udhalilishaji wa abiria kwenye ndege".
Wakati ndege hiyo ilipotua katika mji wa kaskazini wa Manaus, mamlaka ya Brazil iliamuru maafisa wa Marekani "kuzifungua pingu mara moja," Wizara ya Sheria imesema katika taarifa yake.
Mvutano huo mpya kati ya US na Brazil unajiri huku Katibu wa Habari wa Ikulu ya White House ya Marekani akifichua kuwa, katika wiki ya kwanza ya urais wa Donald Trump, wahamiaji 'haramu' 538 wamekamatwa na kuzuiliwa, huku mamia ya wengine wakifukuzwa nchini.
Karoline Leavitt, Katibu wa Habari wa White House amesema kufukuzwa huko ni sehemu ya "Operesheni kubwa zaidi ya kufurusha (wahamiaji) katika historia".
Habari zaidi zinasema kuwa, safari za ndege za wakimbizi zilizotazamiwa kuwasili Marekani karibuni zimefutwa, huku askari wakitumwa kwenye mpaka wa kusini, sambamba na mamlaka husika kuidhinishwa kuwakamata wahamiaji ndani au karibu na shule na makanisa.