Iceland yasisitiza kuendelea shughuli za UNRWA huko Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i122246-iceland_yasisitiza_kuendelea_shughuli_za_unrwa_huko_palestina
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa wa Iceland amesisitiza juu ya udharura wa kuendelea kwa shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hadi utatuzi wa uhakika na wa amani wa mzozo wa Palestina na Israel utakapopatikana.
(last modified 2025-02-02T23:02:15+00:00 )
Feb 02, 2025 23:02 UTC
  • Iceland yasisitiza kuendelea shughuli za UNRWA huko Palestina

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa wa Iceland amesisitiza juu ya udharura wa kuendelea kwa shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu hadi utatuzi wa uhakika na wa amani wa mzozo wa Palestina na Israel utakapopatikana.

Þorgerður Katrín Gunnarsdóttir ameeleza kuwa, "Tunasikitika mno na uamuzi wa  (serikali) ya Israel ya kupiga marufuku UNRWA. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iceland ameongeza kuwa, kuunga mkono shirika hili ni muhimu sana kwa usitishaji mapigano huko Gaza ambao tumekuwa tukiungojea kwa muda mrefu, kutoa msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina na kuendelea kwa utulivu katika eneo hilo.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) litaendelea na shughuli zake licha ya vikwazo vilivyowekwa na utawala wa Israel.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba: "Tunawasiliana na wenzetu wa UNRWA katika kanda ya Asia Magharibi, na wanaendelea kutimiza wajibu wao na kutoa huduma."

Siku ya Alhamisi, Januari 30, Israel ilianza kutekeleza uamuzi wa baraza la mawaziri la utawala huo wa kusitisha shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Jerusalem Mashariki.

Utawala haramu wa Israel umehalalisha hatua yake hiyo kwa kuibua madai yasiyo na msingi kwamba, baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA walishiriki katika Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa dhidi ya vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kambi za kijeshi za utawala huo ghasibu tarehe 7 Oktoba 2023. Hadi sasa Israel imeshindwa kuthibitisha madai hayo.