Papa: Si sahihi kuufananisha Uislamu na utumiaji mabavu
Papa Francis Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani amekosoa propaganda zinazoendeshwa dhidi ya dini ya Uislamu kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni huko Ulaya yaliyodaiwa kutekelezwa na magaidi wa kitakfiri wa Daesh na kueleza kuwa, si haki na ni makosa kuufanisha Uislamu na utumiaji mabavu na ugaidi.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani amesema kuwa afikiri kuwa ni sahihi kuifanisha dini ya Kiislamu na machafuko. Amesema hiyo si haki na si kweli. Papa Francis aliyatamka hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari wakati akitoka Poland kuelekea Italia. Papa Francis alitoa jibu hilo kwa waandishi wa habari baada ya kumuuliza kuhusu kuuliwa mchungaji wa Kikatoliki aliyekuwa na umri wa miaka 86 hivi karibuni nchini Ufaransa. Mchungaji huyo aliuawa kwa kukatwa visu na watu kadhaa walioshambulia misa katika kanisa moja magharibi mwa Ufaransa tarehe 26 mwezi huu.
Kundi la kigaidi la Daesh limedai kuhusika na mauaji hayo ya mchungaji. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani amesema kuwa kila dini ina kundi dogo la watu wenye misimamo ya kufurutu ada na kwamba hata wao wenyewe wana kundi la watu wa aina hiyo. Papa Francis amebainisha kuwa, nchi za Ulaya zinapasa kutilia mkazo masuala yake ya ndani na akataja kukosekana uadilifu wa kijamii na kitendo cha kuabudu pesa kuwa miongoni mwa mambo yanayosababisha ugaidi duniani.