China yaapa 'kupambana hadi mwisho' dhidi ya ushuru wa Trump
(last modified Tue, 08 Apr 2025 09:45:26 GMT )
Apr 08, 2025 09:45 UTC
  • China yaapa 'kupambana hadi mwisho' dhidi ya ushuru wa Trump

Wizara ya Biashara ya China imeionya Marekani dhidi ya kuingia katika msururu wa vikwazo vya kibiashara vya 'kujibishana mapigo' baada ya rais wa nchi hiyo Donald Trump kutishia kuweka ushuru wa ziada kwa bidhaa za China zinazoingizwa nchini Marekani.

Wiki iliyopita, rais wa Marekani alitangaza kuongeza ushuru mpya kwa bidhaa kutoka duniani kote, ikiwa ni pamoja na ushuru wa 34% kwa bidhaa za China. Katika mjibizo iliotoa kwa hatua hiyo, Beijing iliapa kulipiza kisasi kwa kuongeza ushuru wa 34% kwa bidhaa za Marekani zinazoingizwa nchini China na kumfanya Trump atishie kuongeza ushuru mwingine mkubwa zaidi dhidi ya bidhaa za China.

Beijing imelaani kuongezeka kwa vita hivyo vya kibiashara ambavyo imevitaja kuwa ni aina ya "uonevu wa kiuchumi," huku Wizara ya Biashara ya nchi hiyo ikiahidi leo kuwa itachukua hatua madhubuti za kulinda maslahi ya kitaifa ya China.

Msemaji wa wizara hiyo amesema kama alivyonukuliwa na shirika rasmi la habari la China Xinhua: "China itapigana hadi mwisho ikiwa upande wa Marekani umeshakusudia kufuata njia isiyo sahihi".

Wakati huohuo, hisa za Marekani zimeendelea kuporomoka kwa siku ya tatu mfululizo, huku mashirika na wawekezaji wakishindwa kuelewa malengo ya mipango mipya ya ushuru ya rais wa nchi hiyo Trump.

Trump amechochea mvutano na vita vya kibiashara kwa kuweka ushuru mkubwa kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na ushuru wa 10% kwa bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nje na ushuru mkubwa zaidi kwa nchi kama vile China (34%), Umoja wa Ulaya (20%) na Japan (24%). 

Hatua hizo, mbali na kusababisha tetemeko kubwa katika masoko ya fedha duniani na kudhoofisha thamani ya sarafu ya dola ya Marekani, lakini zimezidisha wasiwasi kuhusu mdororo wa uchumi duniani.../