Pentagon yakiri: Kombora la Iran lilitwanga kambi ya US ya Al-Udeid, Qatar
Katika pigo kubwa kwa heshima ya kijeshi ya Marekani, Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo (Pentagon) imekiri kwamba, moja ya makombora ya balestiki ya Iran ilipiga moja kwa moja kambi ya anga ya jeshi la US la Al-Udeid nchini Qatar, wakati wa shambulio la kulipiza kisasi la Tehran mwezi uliopita.
Msemaji wa Pentagon, Sean Parnell ameiambia tovuti ya habari ya Al Arabiya ya Kiingereza kwamba, "kombora moja la balestiki la Iran lililenga kambi ya anga ya Al Udeid" mnamo Juni 23, huku mengine yakizuiwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya Marekani na Qatar.
Amedai kuwa kulikuwa na "uharibifu mdogo" kwa miundombinu ya msingi wakati wa shambulio hilo, lakini alithibitisha kuwa operesheni hiyo ilifanyika.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wakuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Dan Caine, alikiri baada ya shambulio hilo kwamba, "kitu fulani kilipita" ulinzi wao wa hali ya juu, na kulitaja tukio hilo kuwa ushiriki mkubwa zaidi wa kombora la Patriot katika historia ya kijeshi ya Marekani.
Kukiri huko kwa Marekani kunaashiria hatua muhimu katika uwezo wa kimkakati wa kujihami Iran, kwani kombora hilo la Jamhuri ya Kiislamu lilifanikiwa kupenya moja ya ngao imara na muhimu ya kijeshi ya Marekani katika eneo la Al Udeid, kitovu cha operesheni cha CENTCOM, licha ya safu za ulinzi za anga za Washington na washirika wake.
Weledi wa mambo wanasema kuwa, kiteondo cha kombora la balestiki kutoka Iran kukwepa mifumo madhubuti ya ulinzi wa anga ya Marekani na Qatar na kutua ndani ya kambi hiyo, kinatuma ujumbe wenye nguvu kuhusu mapungufu ya ulinzi wa Marekani na ufanisi wa teknolojia ya makombora ya Iran.