Nchi zinazoibukia kiuchumi zimejibu vipi vita vya ushuru vya Trump?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129338
Mataifa matatu yanayoinukia kiuchumi, Brazil, India na Uchina, yamejibu vikali hatua ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ya kupandisha ushuru wa forodha kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.
(last modified 2025-08-09T11:29:46+00:00 )
Aug 09, 2025 11:29 UTC
  • Nchi zinazoibukia kiuchumi zimejibu vipi vita vya ushuru vya Trump?

Mataifa matatu yanayoinukia kiuchumi, Brazil, India na Uchina, yamejibu vikali hatua ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ya kupandisha ushuru wa forodha kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.

Washington hivi majuzi ilitangaza pendekezo la kutoza ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa kutoka Russia na washirika wake wa kibiashara. Wataalamu wa masuala ya uchumi wanaamini kuwa, lengo kuu la Rais wa Marekani katika kuwasilisha pendekezo hilo ni kuziwekea vikwazo nchi tatu ambazo ni Russia, India na China. Uamuzi huo ulifanywa huku Russia ikiendelea kushikilia msimamo wake mkali kuhusu mzozo wa Ukraine, msimamo thabiti wa India katika mazungumzo ya kibiashara na Marekani, na kukataa China kupunguza uhusiano wake wa kiuchumi na Russia.

Huku mvutano kati ya Moscow na Washington ukiongezeka kutokana na vita vya Ukraine, Marekani imeamua kuiwekea vikwazo zaidi Moscow na kuishinikiza Ikulu ya Kremlin ili kumlazimisha Rais wa Putin akubali masharti ya Ikulu ya Rais wa Marekani, hatua ambayo wataalamu wengi wanaamini kuwa hatimaye itakuwa na madhara kwa Washington.

India pia imelaani ushuru wa ziada wa 25% wa Trump - ambaye umeongeza ushuru wa jumla wa bidhaa zinazosafirishwa na nchi hiyo kwenda Merekani hadi 50%. Ushuru huo umewekwa kwa kisingizio kwamba New Delhi imekataa kuacha kununua mafuta ya Russia. India pia imechukua hatua mpya ya kupanua uhusiano na Moscow na kupuuza matakwa ya Trump ya kupunguza uhusiano na Russia. Wizara ya Biashara na Viwanda ya India imetangaza habari ya kutiwa saini mkataba mpya kati ya New Delhi na Moscow wa kupanua ushirikiano wa kiviwanda na kiuchumi katika maeneo muhimu yakiwemo usafiri wa reli, alumini, mbolea na teknolojia ya madini.

China pia imechukua mwelekeo kama huo katika kukabiliana na mashinikizo ya Marekani yanayoitaka kupunguza au kukata ushirikiano na Russia, ikisisitiza udharura wa kukabiliana na mashinikizo ya Washington - ambayo yanatokana na msimamo wa Marekani wa kujichukulia maamuzi ya upande mmoja. Liu Pengyu, msemaji wa Ubalozi wa China nchini Marekani ametangaza kuwa, jaribio la Washington la kuilazimisha Beijing kukata ushirikiano na Russia litashindwa. Amesema: “Vita vya ushuru havina mshindi. Kulazimisha matakwa na mashinikizo naviwezi kufua dafu.”

Liu Pengyu

Washington imeitishia kuiwekea China ushuru wa asilimia 100 na pia inawashinikiza washirika wa kibiashara wa Moscow kuacha kununua mafuta kutoka Russia.

Hii ni katika hali ambayo, sambamba na Marekani kuweka ushuru wa forodha wa asilimia 50 kwa mauzo ya bidhaa za Brazili nchini Marekani – kikiwa kiwango cha juu zaidi kuwahi kuwekwa na serikali ya Marekani -  Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ya Amerika Kusini imewasilisha malalamiko katika Shirika la Biashara Duniani dhidi ya Washington. Ushuru uliotangazwa na Trump ulianza kutekelezwa Jumatano, Agosti 6, 2025. Mashtaka ya Brazil huko WTO ni hatua rasmi ya kwanza ya kukabiliana na ushuru wa 50% wa Donald Trump.

Uamuzi wa serikali ya Marekani dhidi ya bidhaa za Brazil umekosolewa vikali na serikali ya Brasilia na baadhi ya viongozi wa wafanyabiashara wa Brazil wanaoamini kuwa Marekani inataka kuingilia siasa za ndani za nchi yao na kukiuka mamlaka yake ya kitaifa.

Akijibu ushuru wa forodha wa Marekani, Rais wa Brazil, Lula da Silva amesema: "Sasa si wakati wa kufanya mazungumzo ya kibinafsi na Trump na nitashauriana na nchi wanachama wa BRICS juu ya hatua zinazofuata."

Jambo la kuzingatiwa kuhusu visingizio vya Trump vya kutoza ushuru mpya kwa bidhaa za Brazili - zaidi ya visingizio vya kiuchumi – ni uungaji mkono wake kwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Jair Bolsonaro (mmoja wa washirika wake wakuu nchini Brazil). Katika suala hili, da Silva amesisitiza msimamo wake wa kutosalimu amri mbele ya matakwa ya Washington ya kumwachilia huru Bolsonaro.

Lula da Silva

Kwa ujumla, sababu za kushindwa mashinikizo ya Marekani dhidi ya India, Uchina na Brazili kupunguza au kukata uhusiano wa kiuchumi, biashara na mafuta wa nchi hizo na Russia zinaweza kuchunguzwa katika maeneo kadhaa muhimu:

1. Ni maslahi kichumi na usalama wa nishati. Russia inauza mafuta kwa India na Uchina kwa punguzo kubwa, ambalo ni muhimu kwa nchi hizo ili kuweza kudhibiti mfumuko wa bei na kudhamini usambazaji endelevu wa nishati. Uchina na India pia zinahitaji vyanzo vya bei nafuu vya nishati kwa ajili ya ustawi wao wa uchumi na hazina mbadala wa haraka wa mafuta ya Russia. Kukata uagizaji wa mafuta kutoka Russia kunaweza kuzidisha gharama za uagizaji wa India wa bidhaa hiyo kwa dola bilioni 9 hadi 11 kwa mwaka.

2. Sera ya kigeni inayojitegemea. China na India zinasisitiza suala la kujitegemea katika sera zao za nishati na haziko tayari kufuata matakwa ya Washington.

3. Ni uwezo wa kukwepa vikwazo. China inaendelea kukwepa vikwazo na kuagiza mafuta kutoka nje kwa kutumia kundi la meli zisizo rasmi na viwanda vidogo vya kusafisha mafuta.

4. Ni msimamo wa Brazil ambayo ingawa haina uhusiano wa mafuta na Russia kama ilivyo China na India, lakini pia inataka kudumisha uhusiano wa kiuchumi na Russia na kukabiliana na vitisho vya Marekani.

Seneta wa Marekani, Lindsey Graham, ambaye ni mmoja wa viongozi wa Republican katika Seneti ya nchi hiyo, amezitishia nchi hizo kutokana na kushirikiana na Russia, lakini majibu ya nchi hizo tatu yanaonyesha kuwa vitisho hivyo havina meno ya kiutendaji.

Kwa ujumla, nchi hizi zimetanguliza maslahi yao ya kiuchumi na kijiopolitiki kuliko vipaumbele vya Washington, na zimeweza kuhimili mashinikizo ya Marekani kwa kuzingatia nafasi zao kimataifa.